Jeshi la Ethiopia limefanya mashambulizi mapya ya angani katika jimbo la Kaskazini la Tigray katika dalili nyingine ya kuongezeka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. Jeshi la ukombozi wa watu wa Tigray TPLF limesema leo.
Msemaji wa TPLF Gatechew Reda ameandika ujumbe katika ukurasa wa twitter akisema kwamba jeshi hilo lilituma ndege isiyokuwa na rubani katika eneo moja la makaazi la Mekelle usiku wa kuamkia leo.
Reda ameongeza kwamba imekuwa mtindo wa waziri mkuu wa nchi hiyo Abiy Ahmed kulenga maeneno ya makaazi jimboni humo kila wakati jeshi lake linaposhindwa vitani.
Hakuja kuwa na tamko lolote kutoka serikali kuu lakini vikosi vya serikali vilifanya mashambulizi kadhaa katika miji ya Kaskazini mwa nchi hiyo katika wiki za hivi karibuni.
Balozi wa Marekani nchini humo Jeffrey Fatman amekuwa mjini Addis Ababa hadi jana Jumamosi kujaribu kuafikia makubaliano ya kusitisha mapigano.