WAZIRI wa Uvuvi na Mifugo, Mashimba Ndaki ametoa siku 90 kwa minada ambayo haijasajiliwa kufanya hivyo kabla hajaifungia.
Ndaki ametoa maagizo hayo leo katika mkutano wake na Wadau wa Mifugo ambao alikua akisikiliza kero zao ambapo amesema ifikapo Februari 20, 2022 kama kutakua na minada ambayo haijasajiliwa basi ataifunga na kuifuta.
Aidha ameiagiza bodi ya nyama kuchukua hatua za kisheria kwa machinjio, mabucha bubu ambayo yanaendesha shughuli zake bila kufuata taratibu ikiwemo kuwa na kibali.
Pia ameelekeza wanunuzi wa ng'ombe kununua mifugo hiyo kwenye minada ya upili na sio minada ya awali huku akitoa wiki moja kwa madalali kwenye minada kujisajili na kufanya biashara rasmi ya mifugo au kuacha kujihusisha na biashara ya mifugo kwa kuwa hawalipi chochote kwa serikali.
Awali wafanyabiashara wa mifugo wakitoa kero zao kwa Waziri Ndaki walilalamikia utitiri wa kodi wakidai kuwa kuna kodi zaidi ya 20 wanazotozwa toka mikoani hadi kufikisha mfugo mnadani.
"Tunapotoa mifugo kutoka Dodoma kuleta Pugu tunalipa pesa halmashauri, ukifika Pugu unalipia tena, kuna utitiri wa kodi bidhaa moja unalipia zaidi ya mara 10," amesema Joel Meshack, Katibu wa Chama cha wafanyabiashara wa Mazao ya Mifugo Dar es Salaam.
Baadhi ya tozo zilizolalamikiwa ni ile ya leseni, 'service levy' ushuru wa mnada, upakuzi, TRA, Kodi ya Kijiji, wasimamiaji wa ng'ombe, Kodi ya bucha, usafiri wa wanyama na umeme.
Hata hivyo akizungumza suala hilo, Ndaki amesema atazungumza na Ofisi ya Rais TAMISEMI kuangalia namna ya kuondoa baadhi ya tozo kwa kuwa ni nyingi ili kuwapunguzia mzigo wafanyabiashara.
Kero nyingine iliyoelezwa ni mfumo wa usimamizi ambao wafanyabiashara hao wamedai upo sifuri.
"Dar es Salaam ni mkoa ambao wanangalia kukusanya mapato tu na si kuangalia mazingira, ni dampo la kuletwa mifugo hata isiyo na ubora, gredi zote utazikuta kuanzia moja mpaka saba, ukiweza mheshimiwa Waziri pita mitaani utaona masoko na mabucha bubu yamejaa,'" amesema Joel.
Alimuomba Waziri Ndaki, kuwataka watu wake kuwa na usimamizi mzuri ambao utaifanya sekta hiyo izidi kuwa bora na wanaoivamia kufuata taratibu.