Msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov leo ameikosoa Marekani kwa kuchochea wasiwasi kuhusu uwezekano wa Urusi kuivamia Ukraine, baada ya nchi za Magharibi kuishutumu Urusi kwa kuimarisha nguvu zake za kijeshi karibu na taifa hilo lililokuwa la kisovieti.
Akizungumza kupitia televisheni ya kitaifa, peskov aliinyoshea kidole Marekani,akisema hali hiyo ya wasiwasi inazushwa bila ya kuwepo ushahidi na kwamba wale walioleta vikosi vyao vya kijeshi kutoka nje wanaituhumu nchi yake kwamba inaendesha shughuli za kijeshi zisizo za kawaida katika ardhi yao wenyewe.
Matamshi yake yanakuja wakati mataifa ya Magharibi wiki hii yakielezea wasiwasi kuhusu shughuli za kijeshi zinazoendeshwa na Urusi karibu na Ukraine na Marekani kusema ina wasiwasi kuhusu kile ilichokiita shughuli zisizo za kawaida.
Matamshi ya Peskov pia yanakuja baada ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken kukataa jana kusema iwapo idara ya ujasusi ya Marekani inaamini rais wa Urusi Vladimir Putin analenga kuinyakua ardhi ya Ukraine.