EAC Yampa Pole Kenyatta Vifo Vya Watu 32




JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) imetoa pole kwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na wananchi kutokana na ajali iliyotokea mwishoni mwa wiki kwa basi kutumbukia katika Mto Enziu na kusababisha vifo.


Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, hadi sasa miili ya watu 32 imeopolewa.


Barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa EAC, Dk Peter Mathuki kwenda kwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta inaeleza kuwa, EAC imepokea kwa mshtuko taarifa za ajali hiyo iliyoua wananchi wa Kenya na kutoa pole kwa familia na marafiki wa marehemu na majeruhi.


“Tunapongeza juhudi zilizofanywa na wanajeshi pamoja na wadau wengine katika juhudi zao za kuzuia vifo zaidi vya watu na tunawaombea majeruhi kupona haraka,” alisema Dk Mathuki katika barua hiyo kwa Rais Uhuru.


Katika ajali hiyo watu 12 walinusurika kifo wakiwemo watoto wanne.


Waokoaji kutoka Jeshi la Kenya, Polisi, Chama cha Msalaba Mwekundu cha Kenya na Serikali ya Kaunti ya Kitui pia walifanikiwa kupata mabaki ya basi pembezoni mwa Mto Enziu.


"Mabaki ya basi la abiria yametoka kabisa mtoni, miili tisa zaidi imepatikana Jumapili na kufanya jumla ya miili iliyopatikana kufikia 32," alisema Gavana wa Kaunti ya Kitui, Charity Ngilu aliyekuwa akiratibu juhudi za uokoaji.


Basi hilo lilikuwa likipeleka kikundi cha kwaya ya Kanisa Katoliki kwenda kwenye sherehe ya harusi katika Kaunti ya Kitui siku ya Jumamosi wakati lilipozama chini ya maji yaliyokuwa yakitiririka kwa kasi.


Juzi Rais Kenyatta alituma salamu za rambirambi kwa familia za waathiriwa na kuwataka wananchi kuwa waangalifu barabarani wakati wa mvua.


Inaelezwa kuwa, basi hilo lililokuwa limekodishwa linalodaiwa kuwa ni la kubeba wanafunzi lilipokuwa likitaka kupita katika mto huo wapita njia walipiga kelele kumzuia dereva.

Post a Comment

0 Comments