Hali ya ukame nchini Somalia inesemekana kudorora licha ya kuwepo kwa mvua katika baadhi ya maeneo kulingana na afisa wa ngazi ya juu kwenye huduma za kibinadamu za Umoja wa Mataifa Ian Ridley.
Afisa huyo anayeongoza ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kwa ajili ya masuala ya kibinadamu, OCHA nchini Somalia, wakati wa mahojiano na VOA amesema kwamba mvua za hivi karibuni hazitoshi na kwamba ukame umeendelea kushuhudiwa.
Ridley amekuwa akitembelea maeneo yalioathiriwa zaidi katika wiki za karibuni. Wakati akizungumza kutoka mji mkuu wa Mogadishu, Ridley amesema kwamba visima vilivyoko tayari vimeanza kukauka na kwa hivyo kuongeza hitaji la visima vyenye kina kirefu.
Ameongeza kusema kwamba hali iliyoko imelazimisha watu kuhama makwao, baadhi wakisafiri umbali wa kati ya kilomita 30 na 40 kutoka maeneo ya mashambani hadi kwenye maeneo ya mijini.
Amesema pia kwamba kuna hatari kubwa ya kutokea kwa magonjwa kama vile kipindupindu huku surua ikisemekana kuongezeka miongoni mwa watu walioko kwenye makambi.