Sabaya, wenzake wakutwa na kesi ya kujibu


Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imewakuta na kesi ya kujibu watuhumiwa saba wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi akiwAmo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.


Leo Ijumaa Januari 14, 2022 Hakimu Mkazi anayesikiliza kesi hiyo namba 27 ya mwaka 2021, Patricia Kisinda amesema baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi 13 wa Jamhuri na vielelezo 12 mahakama imeona washitakiwa wote saba wana kesi ya kujibu.


Akitoa uamuzi huo mdogo, Hakimu Kisinda amesema baada ya mahakama kupitia vielelezo hivyo na mashahidi vilivyotolewa kuthibitisha makosa yanayowakabili na baada ya kujiridhisha imeona washitakiwa wote wana kesi ya kujibu.


Baada ya uamuzi huo mdogo, Wakili wa utetezi Mosses Mahuna ameieleza mahakama kuwa watakuwa na mashahidi wasiozidi 10 na vielelezo ambavyo hajajua idadi yake na kuomba mahakama iwape muda waweze kujipanga kwa ajili ya kuanza kujitetea.


Hakimu Kisinda ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 17 mwaka huu ambapo watuhumIwa hao wataanza kujitetea.


Mbali na Sabaya watuhumiwa wengine ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.


Washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa matano la kwanza wakidaiwa Januari 22, 2021 ni kuongoza genge la uhalifu na kosa la tano ambalo ni utakatishaji fedha linawakabili washitakiwa wote saba  wanadaiwa kupata Sh 90 milioni kutoka kwa mfanyabiashara Francis Mrosso, huku wakijua kupokea fedha hizo ni zao la kosa la vitendo vya rushwa.


Kosa la pili, tatu na nne Sabaya peke yake ameshitakiwa kwa makosa ya kujihusisha na rushwa ambapo anadaiwa kuchukua Sh 90 milioni matumizi mabaya ya ofisi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro.

Post a Comment

0 Comments