UN: Watu 108 wameuawa Ethiopia tangu kuanza mwaka huu


Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayosimamia haki za binaadamu imesema kuwa takribani raia 108 wameuawa katika mashambulizi ya anga kwenye jimbo la Tigray, Ethiopia tangu kuanza kwa mwezi huu.


Msemaji wa ofisi hiyo, OHCHR Liz Throssell amesema leo kuwa raia hao waliripotiwa kuuawa na wengine 75 wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo yaliyofanywa na kikosi cha anga cha Ethiopia.


Throssell ameyaelezea mashambulizi kadhaa yakiwemo yaliyofanyika dhidi ya basi dogo la watu binafsi, uwanja wa ndege na kambi ya watu wasiokuwa na makaazi. 


Amesema watu wapatao 59 waliuawa katika shambulizi lililofanyika kwenye kambi hiyo na kulifanya kuwa baya zaidi. 


Throssell amewataka viongozi wa Ethiopia na washirika wao kuhakikisha wanawalinda raia kulingana na sheria za kimataifa ambazo zinahitaji uthibitisho kwamba wanaolengwa ni wanajeshi. Amesema serikali ikishindwa kuheshimu sheria hizo kunaweza kuwa uhalifu wa kivita.

Post a Comment

0 Comments