Makumi ya watu wameuawa baada ya watu wenye silaha kuvamia mgodi wa dhahabu huko Djugu katika jimbo la Ituri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo siku ya Jumapili.
Shirika la habari la AFP linamnukuu afisa mmoja wa eneo hilo akisema kuwa miili 29 ilikuwa imetolewa kutoka kwenye mgodi huo. Miongoni mwa waliofariki ni mtoto wa miezi minne, ilisema.
Katika taarifa, wizara ya mawasiliano ililaumu kundi la waasi la Codeco kwa shambulio hilo. "Serikali inabainisha kwamba kitendo hiki cha kumi na moja cha kinyama na cha woga cha magaidi wa Codeco dhidi ya watu wasio na hatia hakitatikisa azma ya kurejesha amani," wizara ilisema.
"Jeshi linafanya kazi usiku na mchana ili kuondoa kabisa makundi yenye silaha hapa Ituri," msemaji wa jeshi alinukuliwa akizungumza na shirika la habari la Reuters. Kundi la Codeco hapo awali limeshutumiwa kwa kufanya uvamizi dhidi ya raia katika miezi ya hivi karibuni. Inalaumiwa kwa kuua takriban watu kumi na wawili kwenye kanisa mnamo Machi, na wengine 60 mnamo Februari.
