Rais wa bunge la Ujerumani Baerbel Bas, amewasili mjini Kyiv leo Jumapili kwa ajili ya kujadili uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na waziri mkuu wa nchi hiyo pamoja na kuadhimisha kumbukumbu ya wahanga wa vita kuu ya pili ya dunia.
Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine mapema leo ametoa hotuba yenye hisia katika kuadhimisha siku ya ushindi, wakati Ulaya inapofanya kumbukumbu ya wanajeshi wa Ujerumani kujisalimisha katika vita hiyo iliopiganwa miaka 77 iliopita.
Baadae hii leo Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz anatarajiwa kushiriki katika majadiliano kwa njia ya video na viongozi wa mataifa ya G7 kujadiliana kuhusu vita vya Ukraine. Ujerumani imekubali kuipatia Kyiv silaha nzito ikiwa ni pamoja na makombora yanayojiendesha yenyewe aina ya Howitzers, baada ya mabadiliko ya sera zake ya kutopeleka silaha katika maeneo ya kivita.
