https://monetag.com/?ref_id=TTIb Utapeli mpya wawaliza wanawake | Muungwana BLOG

Utapeli mpya wawaliza wanawake

 


Ni wimbi jipya la utapeli. Hutokea pale baadhi ya wanawake wanapolazimika kuwalipa fedha waliokuwa wapenzi wao, ili wasisambaze picha zao za utupu kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.


Wimbi hili linaelezwa kuwakumba wajane, wanafunzi vyuoni na wake za watu, ambao kutokana na matatizo ya kifamilia au tamaa za kimwili, huingia katika mtego wa kuwa na uhusiano nje ya ndoa, huku wakipiga picha bila kufahamu zitatumikaje hapo baadaye.


Wahusika wakubwa ni vijana wa kiume wenye kipato cha kati ambao wanakuwa kwenye uhusiano na wanawake wenye uwezo wa kutoa fedha wanazozitaka.


Uchunguzi wa Mwananchi umebaini baadhi ya wasichana na wanawake wanaingia kwenye uhusiano na watu waliokutana nao kwenye mitandao ya kijamii.


Mjini Moshi

Taarifa zinasema kuna vijana wanaoshinda kwenye klabu za mazoezi (Gym) kujenga miili ili kuvutia wanawake, wakiamini wanapokwenda kufanya nao mapenzi huwa ni watu wenye nguvu zaidi.


Uchunguzi wa gazeti hili katika mji huo, umebaini mtandao wa vijana hao unaohusisha wahudumu wa saluni ambao huwaunganisha na wasichana na wanawake wenye fedha, wakiwamo wake za watu.


Pia kundi hilo la vijana huwalenga wanawake wajane ambao waume zao wamewaachia utajiri. Kupitia mipango ya wasichana wa saluni, wanawake hao hujikuta wameingia mtegoni.


“Hao vijana ni wa matanuzi (wapenda starehe) sana kwenye klabu, huwatumia sana kinadada wa saluni kuwatongozea wake za watu, kinamama na wasichana wenye uwezo; hufanya kila njia wawapige picha ambazo wanazitumia kutapeli,” ilielezwa.


Taarifa zinasema katika mji huo, kumeanza kuibuka matukio ya ajabu ajabu ya ulipizaji wa visasi, lakini kikifuatiliwa kiini cha matukio hayo, inagundulika ni ama kijana alitembea na mke wa mtu au kutapeli fedha kupitia picha hizo.


“Inauma sana, yaani unamhudumia mke wako vizuri halafu anatokea kijana mpuuzi tu anaunganishiwa dili na hao wasichana wa saluni, unadhani mwenye mume atamwacha?” alihoji mkazi mmoja wa Moshi, ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake.


Taarifa ambazo Mwananchi inazo ni kwamba wapo wanawake wa mkoani Kilimanjaro wenye uwezo wa kifedha, wakiwamo wake za watu na wajane, walioingia katika mtego huo wa uhusiano wa kitapeli, lakini wanaogopa kulalamika wakihofia aibu na ndoa kuvunjika.


Jijini Dar es Salaam

Mkazi wa Kinondoni, Abubakar Twaha anawahusisha vijana wanaojenga miili yao na utapeli huo, kwa sababu wamekuwa wakitumia muda mrefu kufanya mazoezi badala ya kazi.


“Unamkuta kijana yuko gym asubuhi mpaka jioni anafanya mazoezi ya kujenga kifua, ili avutie wanawake. Sasa huwa najiuliza hawa wanafanya kazi saa ngapi? Si ndiyo wale wale unaowazungumzia?


“Ikifika usiku wako baa, kama siyo majambazi basi kazi zao ndiyo hizo za utapeli wa mapenzi,” anasema mkazi huyo na kutahadharisha jamii dhidi ya vijana hao.


Simulizi ya Briyanca

Briyanca Travis (si jina halisi) ni mmoja wa waathirika wa wimbi hilo, jambo ambalo lilimfanya kupoteza kazi na kupata msongo wa mawazo.


Akiwa mwanafunzi wa mwaka wa pili katika chuo kimoja jijini hapa alianzisha uhusiano wa kimapenzi na mwanamume aliyekuwa akiishi Sweden baada ya kukutana naye katika mtandao wa Facebook.


“Alinitumia fedha bila kuomba, pesa haikuwa shida kwake, ila sikujua nini kitatokea baadaye,” anasimulia Briyanca.


Anasema baada ya uhusiano wao kudumu kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja na nusu, mwanamume huyo alikuja jijini Dar es Salaam ambapo hakuwa na mashaka naye.


“Aliniondolea woga siku ya kwanza, tulilala wote na hatukukutana kimwili, mara ya pili alivyokuja pia ilikuwa hivyo, lakini alisema yote ni kwa sababu ananipenda,” anasema Briyanca.


Jambo hilo lilimfanya aongeze mapenzi zaidi, kwani lilimfanya kuona ndiye mwanamume sahihi kwake na hata ilipofika hatua ya kuanza kuombwa picha za utupu haikuwa shida, kwani kila alichokiomba alipewa.


“Nilimtumia picha nyingi sana, mara ya tatu alipokuja aliniomba tufanye mapenzi akitaka kurekodi, niligoma, akasema ananipenda, akiwa mbali anataka aangalie picha zangu.


“Nilikubali kwa sharti asichapishe picha hizo sehemu yoyote, akakubali,” anasimulia Briyanca.


Kibao chageuka

Siku chache baada ya mwanaume huyo kurudi Sweden, alimpigia simu na kumuomba Sh1 milioni na kama asingefanya hivyo picha na video zake zingesambazwa mtandaoni.


Alilazimika kuzituma ila maombi ya fedha yalizidi yakiambatana na vitisho, jambo lililomfanya dada huyo kuingia katika mikopo.


“Yote haya yakifanyika nilikuwa na mawazo, kazini utendaji wangu ukashuka, mwili ukaisha, naugulia mwenywe mwisho walio karibu yangu walinibana ili kujua shida ni nini.


“Baada ya kupata ushauri nasaha, na kuelezwa namna gani naweza kumuepuka, mwishowe nilichukua uamuzi wa kum-block (kumkatia mawasiliano) kila sehemu mitandaoni hata kwenye namba za kawaida.


“Namba ya simu anayoijua nikaitupa nikasajili mpya, huku nikiwa nawaza endapo nitakutana na picha hizo mitandaoni itakuwaje. Ikapita wiki, mwezi, mwaka na sasa ni miaka mitatu, nimeolewa na mtoto mmoja ila ni kitu ambacho siwezi kukisahau,” anasimulia Briyanca.


Hali ilivyo vyuoni

Akifafanua namna wanavyoshughulikia mikasa hiyo vyuoni, Rais wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Paul Godwell anasema matukio kama hayo yamekuwa yakiwakuta wanafunzi wa vyuo.


Godwell anasema mazingira hayo hutokea kwa watu kuahidiwa pesa, na kwamba kibao hugeuka akitakiwa alipe ili asidhalilishwe.


“Kwa sababu uhitaji mkubwa huwa ni pesa, kama chuo tunacho kitengo maalumu cha ushauri kwa wanafunzi ili kuwasaidia kuondokana na msongo wa mawazo. Mtu akiwa katika hali hiyo yuko tayari kufanya chochote ili apate fedha,” anasema.


Godwell anasema kitengo hicho kina mfuko wa kuwasaidia wanafunzi kwa kiasi kidogo ili kuwaepusha kuingia katika matatizo pale wanapoonekana kuwa na uhitaji mkubwa, na hilo hufanyika wa ushirikiano na taasisi mbalimbali na makanisa.


Kauli ya polisi

Kamanda wa Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro anawashauri watu wa namna hiyo kuripoti polisi, ili wafanye uchunguzi na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.


Hata hivyo, anasema hajawahi kusikia kesi za aina hiyo, lakini anawahimiza wanaokabiliwa na matukio kama hayo kutoa taarifa polisi, badala ya kuamua kumalizana na wanaohitaji fedha kutoka kwao.


“Kesi tunazozijua ni za kweli, mtu anahitaji msaada wa kisheria, anaripoti polisi, sasa usije ukajikuta unashughulika na kesi za kufikirika.


“Hata nyie mkisikia mtu anaelezea, muulize umewahi kuripoti wapi? Kwa nini hutaki kuripoti? Kwa nini utake hela, kwa nini utoe hela. Unaweza ukadhani una kesi, kumbe ni ya kufikirika,” anasema Kamanda Muliro.


Mwanaharakati afunguka

Mwanaharakati Carol Ndosi ambaye pia amekuwa akishughulikia kesi za aina hii, anasema mara nyingi utegemezi wa kiuchumi wa wanawake kwa wanaume ndio umekuwa ukiwafanya watume picha zao za utupu wakidhani wanawavutia wanaume, jambo ambalo si kweli.


Anasema baadhi ya wanawake wanatuma picha hizo bila kuombwa, jambo ambalo wakati mwingine wanaume hulazimika kuomba msaada wa watu kuzungumza nao ili waache.


“Kuna mwathirika mmoja alikuwa mwanafunzi wa chuo, aliona maisha wanayoishi wenzake akatamani na akawa anatoka na mume wa mtu bila kujua. Alipangiwa nyumba, akanunuliwa na gari, alipokuja kujua akaona ajiondokee,” anasema.


Anasema mwanamume akawa anakataa na kumwambia akimuacha atasambaza picha zake za utupu kwa madai kwamba haiwezekani amhudumie miaka mingi halafu amwache kirahisi.


Carol anasema hilo halitokei kwa wanafunzi tu, bali hadi watu wazima, kwani wamekuwa wakikutana na hali hiyo, japo anasema waathirka wakubwa ni wasichana wa kati ya miaka 18 hadi 27.


“Wengi wao yakishawakuta wanataka kujitoa uhai, kutokana na kudhalilishwa kwa ndugu na jamaa,’’ anaeleza.


Anasema inapotokea hali kama hiyo ya mtu kutaka kujiua hufanyiwa kwanza ushauri wa kisaikolojia ndiyo hatua nyingine zinafuata.


“Mpaka sasa tumeshapokea kesi zaidi ya 220 tangu mwaka 2020,” anasema Carol.


Anasema kwa bahati mbaya, kesi hizi hakuna hata moja iliyoweza kufika katika ngazi ya mahakama na wakati mwingine zimekuwa zikikwama vituo vya polisi.


“Wanakwambia hebu tupe namba ya huyo mwanamume tumpigie tuongee naye wakati hilo siyo jukumu la polisi na badala yake wanatakiwa kupokea kesi na kuzifanyia uchunguzi,” anaeleza.


Anaongeza: “Wengine wanaokutana na hizi changamoto hawawezi kuendelea na kesi kwa sababu hawana uwezo wa kumudu gharama za mwanasheria, walipokuja kwetu tukawapa msaada wa kisheria kupitia Wildaf,” anasema.


Anatolea mfano wa kesi ambayo wanafunzi wengi wa vyuo walidanganywa kuwa wakituma video zao za utupu watanunuliwa iPhone 13 na Sh700,000, jambo ambalo halikufanyika na baadaye video zao zilisambaa mitandaoni.


Wanasaikolojia washauri

Mwanasaikolojia Charles Nduku anasema chanzo cha mambo haya ni kufanya jambo kabla halijawa la kudumu, akisema mara nyingi visa vya namna hiyo vinatokea kwa watu wasio wanandoa, hivyo mmoja haoni cha kupoteza.


Anasema ni muhimu watu wakachukua tahadhari wanapowatumia wenzao picha za utupu za namna yoyote ile, kwamba baada ya kumtumia mamlaka ya matumizi inabaki kwa mtumiwaji na aliyetuma hana uwezo tena wa kudhibiti.


“Inawezekana hata kabla ya kuanza kukutisha kuzisambaza tayari alishawatumia watu wake wa karibu bila wewe kujua na hiyo imekuwa ikitokea sana. Muhimu ni kutofanya hicho kitu kama huna uhakika na upande wa pili,” anasema.


Anasema kwa watu wenye uhusiano rasmi ni rahisi kuchukua hatua, lakini pia hata kuchunguza na kutoa ushahidi usio na shaka.


“Sasa hivi watu wanatumia mambo haya kama njia ya kujipatia kipato, kunyanyasa wengine, kutishana na kupeana masharti, mwisho wanaofanyiwa wanajikuta wakiingia kwenye msongo wa mawazo na wengine kuona hakuna thamani ya maisha hadi kutaka kujiua,” anasema Nduku.


Imeandikwa na Peter Elias, Aurea Simtowe na Ephrahim Bahemu (Dar es Salaam) na Daniel Mjema (Moshi).

Post a Comment

0 Comments