Ticker

6/recent/ticker-posts

 


Walioathiriwa na tembo Nachingwea kufutwa machozi

 


Na Ahmad Mmow, Nachingwea.

Wakulima ambao mashamba yao yalivamiwa na kuharibiwa mazao yao ya kilimo na tembo wameombwa wajiorodheshe ili wapate kifuta machozi.

Wito huo ulitolewa jana kijijini Kitandi wilayani Nachingwea, mkoa wa Lindi na mkuu wa idara ya maliasili wa halmashauri ya wilaya ya Nachingwea, Lington Nzunda apozungumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji hicho.

Nzunda alisema wakulima wote ambao mazao yao yameharibiwa na kuliwa na ndovu hawanabudi kujiorodhesha ili walipwe kifuta machozi( fidia). Kwani ni dhamira ya serikali kuona wakulima hao wanapata kifuta machozi.

Aliwaasa wakulima wa kijiji hicho na wengine waliopo wilayani Nachingwea ambao mshamba yao yameharibiwa na  tembo wakamilishe zoezi hilo haraka kabla ya tarehe 31.06.2022.

" Jiorodhesheni ili majina yenu yafikishwe kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya yaweze kupelekwa Dodoma. Msije kulalamika na kulaumu baadae kama hamtajiandikisha," Nzunda alisisitiza na kuonya.

Kwaupande wake mkuu wa wilaya ya Nachingwea, Hashim Komba aliwaasa wakulima wilayani humo wazingatie na kufanyia kazi maelekezo ya maofisa wanyama pori juu ya kujilinda na kulinda mashamba yao dhidi ya tembo.

Alisema kama watazingatia na kufanyia kazi maelekezo ya maofisa wanyama pori wataweza kujilinda na kulinda mashamba yao kuharibiwa. Ikiwemo kupanda pilipili kuzunguka mashamba yao.

Hivi karibuni maofisa na askari wa mamlaka ya usimamizi wanyamapori nchini(TAWA) wamekuwa wakitoa elimu ya jinsi ya kujilinda na kulinda mashamba dhidi ya tembo katika maeneo mbalimbali nchini ikiwamo katika wilaya ya Nachingwea.

Post a Comment

0 Comments