Ticker

6/recent/ticker-posts

Wabunge na Watumishi wa Bunge 39 wahitimu mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria

 


Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.

Wabunge na watumishi wa Bunge wapatao 39 ikiwa wabunge 21 na watumishi 18 wamehitimu mafunzo ya jeshi la kujenga taifa JKT kwa mujibu wa sheria yaliyopewa jina la oparetioni jenerali  Venance Mabeyo mafunzo yenye lengo la kuwajengea uzalendo na uhodari katika utendaji kazi.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo Mkuu wa Utumishi jeshi la ulinzi la wananchi Tanzania JWTZ Meja Jenerali Paul Kisesa Simuli amesema mafunzo hayo yaliyofanyika kikosi cha 834 KJ Makutopora yamelenga kuwajengea vijana  uwajibikaji,uhodari, uzalendo, ukakamavu na stadi za maisha.

“Nitumie nafasi hii kuwapongeza kwa dhati kabisa wabunge na watumishi wa bunge mliofanya maamuzi haya ya kizalendo na kijasiri kwa kuacha shughuli zenu na kuja kwenye mafunzo haya mmefanya maamuzi magumu” amesema.

Amesema kitendo cha kuhudhuria mafunzo hayo kunawafanya kuwa wakakamavu, wazalendo, watii na wenye Moyo wa utayari wa kufanya kazi katika mazingira yoyote na nina amini mara baada ya kurudi majimboni utandaji kazi utabadilika.

“Nimepata taarifa kuwa mbali na kujifunza masomo ya darasani na medani pia mmeshiriki katika shughuli za ujasiliamali na tunaamini haya mliyoyapata yatakuwa msaada mkubwa kwenu katika utendaji kazi wenu” amesema.

Amelishukuru Bunge kwa kuwapa nafasi wabunge na watumishi kuhudhuria mafunzo hayo ikiwa ni hamasa kwa vijana kuhudhuria mafunzo hayo na kuzitaka taasisi nyingine kuwapeleka watumishi wao kuhudhuria mafunzo hayo na kujenga uzalendo na mshikamano kazini kwa maendeleo ya taifa.

Awali Mkuu wa kikosi cha 834 KJ Makutopora Luteni Kanali Festo Mbanga amesema mafunzo hayo yalikuwa ni ya majuma manne ambayo yalianza jully 5 hadi august 5, 2022 yakihusisha watumishi na wabunge 39.

“Walianza wakiwa 39 na wamemaliza 39 huu ni ujasiri mkubwa na ninajua kabla ya kuja hapa mlipata maneno ya kupotosha lakini mlipuuza na leo mmehitimu salama niwaombe na wengine wasiogope maneno ya watu waje wajifunze uzalendo” amesema.

Akizungumzia mafunzo waliyopewa amesema ni matumizi ya silaha ndogo ndogo, kwata, mbinu za kivita, ujanja wa porini, utimamu wa mwili, uraia na uzalendo, huduma ya kwanza, usomaji ramani, usalama na utambuzi.

Mengine ni mazoezi ya medani, ulengaji shabaha, masomo ya uzalishaji mali ambapo wamejifunza kilimo kuandaa bustani za mbaga mboga na ufugaji wa kuku kwa lengo la kujiongezea kipato ambayo huwasaidia vijana katika kupata kipato baada ya kumaliza mafunzo.

Amesema wanaamini kitendo cha wabunge kukubali kuhudhuria mafunzo hayo kinayaongezea thamani mafunzo hayo ambapo vijana wengi wataanza kuja kupata mafunzo hayo.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT Kanali Erasmus Bwegoge amewashukuru wabunge waliojitoa kupata mafunzo hayo na kuwapongeza wakufunzi wa mafunzo na wanaamini kwa paredi waliyopiga mafunzo hayo yamewaingia.

Amesema kupitia mafunzo hayo yatawasaidia katika kuwa wazalendo na wavumilivu katika majukumu yao hasa katika kutunga sheria na katika kuwawakilisha wananchi wao Bungeni.


Nao baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo akiwamo mkuu wa wanafunzi wa kozi maalumu ya wabunge na watumishi wa bunge Agnes Ndumbati amesema wamenufaika na mafunzo hayo wamejifunza mambo mengi ikiwamo utii hasa kwa viongozi.

Aidha amewataka watumishi wengine kuja kwenye mafunzo hayo kwani yanamanufaa makubwa katika utendaji kazi wao pia amewapongeza viongozi wa bunge kwa kuwapa ruhusa ya kuhudhuria mafunzo hayo.

Post a Comment

0 Comments