Ticker

6/recent/ticker-posts

Malori ya mizigo yakwama katika mpaka wa Uganda na DRC kutokana na ukosefu wa usalama mashariki mwa DRC

Mamia ya malori ya mizigo yamekwama upande wa Uganda kwenye kivuko cha mpaka cha Ishasha, huku mapigano yakipamba moto mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.


Sostine Buregyeya, kiongozi wa eneo hilo na mfanyabiashara huko Ishasha, ameambia BBC kwamba baadhi ya lori hizo zimekwama mpakani kwa wiki tatu, kwa hofu ya ukosefu wa usalama ndani ya D R Congo.


Mauzo ya Uganda kwenda DRC yana thamani ya zaidi ya dola za Marekani milioni 300, na Ishasha ni mojawapo ya njia kuu kati ya nchi hizo mbili."Tulikuwa tukienda DRC mara mbili kwa mwezi, lakini sasa hakuna biashara,"


Geoffrey Opiyo, msafirishaji samaki kutoka Uganda aliambia BBC.


Bw. Opiyo alisema kuwa amelazimika kuuza baadhi ya shehena zake za samaki waliokaushwa hapa nchini kwa bei ya chini na bado amekwama na tani 40 kwenye duka mpakani.


Alileta shehena mpakani, akisafiri kutoka Ziwa Kyoga la Uganda mashariki, mwishoni mwa Oktoba.


"Baadhi ya malori ambayo tayari yalikuwa yamevuka yamerejea Uganda," Bw. Opiyo aliongeza.


Mapigano kati ya serikali ya Kongo na waasi wa M23 yamezidi katika wiki za hivi karibuni, huku waasi hao wakiteka maeneo zaidi.


M23 wanasemekana kusonga mbele katika maeneo kadhaa, na wameonekana takriban kilomita 35 kutoka mpaka wa Ishasha.


Waasi hao pia wamekuwa wakisonga mbele kuelekea mji wa kimkakati wa Goma.


Mapigano hayo yamewakosesha makazi maelfu ya watu katika eneo hilo.


Juhudi za kuleta amani mashariki mwa DRC zinaungwa mkono na viongozi wa jumuiya ya Afrika mashariki, pamoja na rais wa Angola Joao Lourenco ambaye anaandaa mkutano katika mji mkuu Luanda siku ya Jumatano.

Post a Comment

0 Comments