Waziri Prof. Mkenda akutana na wamiliki wa shule binafsi

 


Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda amekutana na Wamiliki wa shule binafsi hapa nchini huku akiwataka wamiliki hao kusimamia maadili katika shule zao na kuwataka kutoa taarifa mapema kwenye mamlaka husika wanapobaini viashiria vya vitendo visivyo vya kimaadili.

Pia amewataka wamiliki wa shule binafsi pamoja na wadau wengine kuipitia rasmu ya maboresho ya sera ya elimu pindi itakapotoka ili pindi itakapo pitishwa tayari kwa utekelezaji kusiwe na malalamiko.

Akizungumza kwenye kikao hicho Waziri Prof. Mkenda  amesema  suala la maadili lazima liangalie kwa ukaribu na kufanyiwa kazi mapema ikiwa ni pamoja na kuwafichua watu wanaofanya vitendo hivyo.

”Wamiliki simamie malezi kwa wanafunzi wetu katika shule zenu  ili kuendelea kutoa kizazi chenye maadili na kuondokana matukio mabaya yanayoripotiwa katika baadhi ya shule kuwa kuna mafundisho yanayotolewa ya tabia chafu.”amesema Prof.Mkenda

Ameongeza kuwa “Tupo katika maboresho ya sera ya elimu na muda si mrefu rasmu itatoka ili wadau waisome ni vizuri na ninyi mkaipitia kwa makini ili kama inahitaji maboresho mengine au kuongezwa baadhi ya vitu” amesema.

Sambamba na hilo Prof. Mkenda amewataka wamiliki wa shule kuwa makini na vitabu vinavyotolewa kama misaada kuwa ni lazima vichunguzwe kwa umakini kabla ya kuanza kutumika katika shule zao.

 “Tunayo maadili yetu ambayo lazima tuyalinde na kuyasimamia yasipotee, hata vitabu vinavyotumika lazima sasa vikaguliwe kabla ya kuanza kutumika ili kuondokana na matumizi ya vitabu ambavyo havina maadili kwa jamii yetu,”amesema. 

Hata hivyo Waziri  Mkenda amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na shule binafsi katika kuinua na kuendeleza sekta ya elimu hapa nchini.

“Niwatoe wasiwasi kuwa Serikali inatambua na inathamini mchango wenu katika maendeleo ya sekta ya elimu hapa nchini hivyo msifikirie kwamba tumewaacha nyuma hapana tunawahitaji sana muendelee kuwekeza katika Elimu yetu,”amesema Prof.Mkenda

Pia Waziri Mkenda amesema kuwa  suala la wizi na uvujishaji wa mitihani ni jinai na kutangaza kuwachukulia hatua watendaji, wasimamizi, walimu na wote watakaothibitika kuhusika katika jambo hilo na kusababisha shule binafsi zipatazo 22 kufungiwa vituo vya mitihani.

“Mitihani ni gharama katika shule hizo kulikuwa na wasimamizi wa mitihani, vyombo vya ulinzi na usalama  ikiwemo, watu kutoka taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa(TAKUKURU), Polisi, usalama wa Taifa, Baraza la mitihani, labda niwambie tatizo hilo la wizi wa mitihani halipo kwenye shule binafsi pekee lipo hata shule za Serikali,”amesema Mkenda.

Katika hatua nyingine Prof. Mkenda amesema Wizara itapitia suala la wingi wa tozo ambao umekuwa ukilalamikiwa na wamiliki na wadau wa shule binafsi ili kuendelea kuvumia wawekezaji wengine katika kuendesha shule.

Kwa upande wao Wamiliki wa Shule binafsi wamemuomba Prof. Mkenda katika bajeti ya Wizara ijayo kuongeza bajeti ya kuwalipa idara ya Uthibiti Ubora wa Shule wakati wanakwenda kutekeleza jukumu la kukagua shule kwani imekuwa ikiwaumiza kulipa ili waende kukaguliwa.

Pia Wamiliki hao wameomba kuondolewa kwa gharama za Mitihani kwa wanafunzi wanaosoma katika shule binafsi kwani hawana tofauti na wanafunzi wanaosoma shule za Serikali ambao wao wamefutiwa gharama za mitihani.

 

 

 

Post a Comment

0 Comments