https://monetag.com/?ref_id=TTIb Mkuu wa JKT azindua mitambo mikubwa ya kuzalisha zege ya SUMAJKT | Muungwana BLOG

Mkuu wa JKT azindua mitambo mikubwa ya kuzalisha zege ya SUMAJKT

 Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.

Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT Meja Jenerali Rajabu Mabele amezindua rasmi mitambo mikubwa ya kuzalisha na kusafirisha zege itakayokuwa ikitumiwa na kampuni ya ujenzi ya Shirika la uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa SUMAJKT iliyogharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.349 za kitanzania.

Akizungumza mara baada ya kuzindua mitambo hiyo Meja Jenerali Rajabu Mabele amewaagiza watendaji wa SUMA JKT kuhakikisha wanasimamia mitambo hiyo ili ilete tija iliyokusudiwa katika kuongeza ufanisi wa SUMAJKT.

“Kwa watakao pewa dhamana ya kusimamia mitambo hiyo lazima wazingatie matengenezo kwa wakati ili mitambo hiyo idumu kwa muda mrefu sio ukiona mtambo unafanya kazi unaendelea kuutumia hali ukijua muda wa matengenezo umefika” amesema.

Amebainisha kuwa JKT inakwenda kuadhimisha miaka 60 tangu kuasisiwa  kwake na sasa ni wakati wa teknolojia ni lazima tuonyeshe mabadiliko kwa kuwa na vifaa vya kisasa katika kutekeleza majukumu.

“Kama mnavyojua SUMA JKT ilianza kama kitengo cha ukarabati lakini kilikuwa na sasa ni shirika kubwa sana hapa nchini na linaloaminika na linalopata miradi mikubwa lazima tuonyeshe utofauti.

Mwanzo tulikuwa tunaingiza vijana wengi mashambani lakini kwa sasa tumeweka mitambo mikubwa ya kiteknolojia mashambani na tunalima kwa tija kubwa kutokana na mitambo tuliyonayo” amesema.

Amesema mwanzo shirika lilikuwa likiingia gharama kubwa katika kununua zege na kokoto na kwa sasa shirika linajitegemea kwa mitambo na mwerekeo ni kuendelea kununua mitambo mingine na krasha ya kutengeneza kokoto ili kuendelea kupunguza gharama za uendeshaji wa shirika.

Ameongeza kuwa “tunaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuiamini SUMAJKT kwa kuipa miradi mingi na ndio maana wanapambana kuhakikisha wanapata mitambo ili kutekeleza miradi hiyo kwa ufanisi na tutaendelea kuilinda imani hiyo” amesema.


Awali msimamizi wa miradi ya ujenzi SUMAJKT Mhandisi Mogan nyoni amesema mitambo hiyo imeingizwa nchini Januari 16, 2023 na kumaliza kusimikwa May 22, 2023 jijini Dodoma, na inauwezo wa kuzalisha zege cubic meter  60 kwa saa, magari matatu yenye uwezo wa kubeba zege cubic meter 8 kila moja na pampu ya kusukuma zege.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa SUMAJKT Kanali Petro Ngata amesema mitambo hiyo itasaidia katika kutekeleza miradi wanayopata na wamejiwekea malengo ya kuongeza vitendea kazi kwa kampuni tanzu za SUMAJKT kuziwezesha kampuni hizo ufanisi katika kutekeleza majukumu yao.

Ameongeza kuwa “ Mwanzo tulikuwa tukinunua zege katika kutekeleza miradi yetu lakini sasa tutatumia mitambo yetu kuzalisha zege na tutaweza kuhudumia makampuni mengine ya ujenzi katika jiji la Dodoma” amesema.


Nae mwenyekiti wa bodi ya washauri wa SUMA JKT Meja Jenerali Mstaafu Farah Mohamed ameipongeza SUMA JKT kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kutekeleza yote wanayokubaliana katika vikao vya bodi na Shirika hilo.

Post a Comment

0 Comments