Gabon imeondolewa kwa muda katika Jumuiya ya Madola baada ya makamanda wa kijeshi kufanya mapinduzi yaliyomuondoa madarakani Rais Ali Bongo.
Uamuzi huo umetolewa na mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Madola waliokutana pembezoni mwa mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Viongozi walitoa wito kwa Gabon kuzingatia maadili na kanuni za Jumuiya ya Madola.
Waliomba nchi kufanya uchaguzi wa kuaminika haraka iwezekanavyo.
Jeshi la Gabon lilimwondoa Bw Bongo mamlakani muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais wa 2023.
Bw Bongo amekuwa akiongoza nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta tangu 2009, alipomrithi babake ambaye alitawala kwa miaka 41.
Awali aliwekwa chini ya kifungo cha nyumbani huku viongozi wa kijeshi wakichukua hatamu za uongozi, lakini baadaye aliachiliwa na kupewa ruhusa ya kusafiri nje ya nchi kwa uchunguzi wa kimatibabu.
