Vita vya Israel na Gaza: Wakazi wasema Israel imefanya mashambulizi makubwa zaidi tangu kuanza kwa vita


 Israel imefanya mashambulizi makali ya anga dhidi ya Khan Younis kusini mwa Gaza, huku wakazi wakieleza kuwa ni mashambulizi makali zaidi ya kivita katika vita hivyo.


Watu katika maeneo ya mashariki mwa mji huo wameambiwa na jeshi la Israel kuhama zaidi kuelekea kusini.


Israel inaamini baadhi ya viongozi wa Hamas wako katika mji huo, ambapo raia wengi wanajihifadhi baada ya kutoroka kaskazini.


Wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas imesema takribani watu 193 wameuawa katika mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel.


Siku ya Ijumaa, Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) lilianza tena mashambulizi yake dhidi ya Hamas huko Gaza, iliyoanzishwa kujibu mashambulizi ya Oktoba 7 huko Israeli ambayo yaliua karibu watu 1,200.


Wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas inasema idadi ya watu waliouawa Gaza sasa imezidi watu 15,200.


Mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza yalianza tena baada ya kusitishwa kwa muda kwa mapigano siku ya Ijumaa.


Makombora pia yamekuwa yakirushwa mara kwa mara dhidi ya Israel kutoka Gaza tangu mapigano yalipoanza tena, ikiwa ni pamoja na mashambulizi yaliyolenga Tel Aviv na eneo jirani la Israel ya kati Jumamosi jioni.


Kufuatia shambulio hili, huduma ya kubeba wagonjwa ya Israel ilisema ilimtibu mwanaume mwenye umri wa miaka 22 "majeraha madogo ya risasi" kichwani huko Holon, mji ulio kusini mwa Tel Aviv.


Katika kikao fupi Jumamosi jioni, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliahidi kuendelea na operesheni ya kijeshi ya Israel hadi "watakapofikia malengo yote" ya kuwaondoa Hamas na kuhakikisha kuwa mateka hao wameachiliwa.


Alikiri kwamba "vita vikali viko mbele yetu". Khan Younis na mji wa Rafah, kwenye mpaka na Misri, ni baadhi ya maeneo ambayo yamekumbwa na mashambulizi makali ya anga, huku awamu inayofuata ya mashambulizi hayo yakielekea kulenga kusini mwa Gaza.


Mamia kwa maelfu ya Wapalestina wametafuta hifadhi katika eneo hilo, baada ya kuambiwa wakimbie kaskazini mwa ardhi hiyo, ambayo ndiyo ilikuwa shabaha kuu ya Israel katika hatua za mwanzo za vita.


Msemaji wa IDF kwa lugha ya Kiarabu alichapisha ramani kwenye mitandao ya kijamii ikionesha ni maeneo gani raia wanapaswa kuondoka, akielekeza watu katika maeneo ya mashariki ya Khan Younis kuhama kusini zaidi hadi kwenye makazi huko Rafah.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items

Kilimo cha Bamia