Watu watatu wameuawa na tisa kujeruhiwa katika mlipuko uliotokea wakati wa misa ya Kikatoliki nchini Ufilipino, maafisa wanasema.
Kisa hicho kilitokea katika ukumbi wa mazoezi katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Mindanao (MSU) katika jiji la Marawi Jumapili asubuhi.
Mnamo mwaka wa 2017, jiji hilo lilikuwa uwanja wa vita vya miezi mitano kati ya vikosi vya serikali na wanamgambo wenye uhusiano na Islamic State.
Chuo kikuu kilisema "kimehuzunishwa sana na kushangazwa" na ghasia hizo "zisizo na maana na za kutisha". "Vurugu hazina nafasi katika jamii iliyostaarabika, na ni jambo la kuchukiza sana katika taasisi ya elimu ya juu kama MSU," ilisema.
"Tunasimama kwa mshikamano na jumuiya yetu ya Kikristo na wale wote walioguswa na janga hili."
Chuo hicho kiliongeza kuwa wafanyakazi wa ziada wa usalama wametumwa katika chuo chake na kwamba shughuli zote za masomo zitasitishwa hadi taarifa nyingine itakapotolewa.
