Profesa Janabi: Matumizi makubwa ya chumvi chanzo cha magonjwa

Na John Walter -Arusha
Matumizi ya Chumvi yaliyopitiliza kwa kuzidisha kiwango kinachoshauriwa,  yametajwa kuwa sababu kuu ya magonjwa yasiyoambukiza kwa wakazi wa Arusha ikiwemo shinikizo la juu la damu, kiharusi na magonjwa ya moyo.

Haya yameelezwa na Profesa Mohamed Janabi, Daktari bingwa wa moyo na Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya Taifa Muhimbili alipokuwa akizungumza na wanahabari kwenye kambi ya Madaktari bingwa na wabobezi inayoendelea kwenye Mkoa wa Arusha leo Alhamisi Juni 27, 2024.

"Chumvi inatoa maji yaliyokuwa ndani, inaingiza kwenye mzunguko. Ukiongeza kiwango cha maji kwenye mzunguko, Presha inakwenda juu sasa Presha za Arusha zinatia wasiwasi kama hatukuchukua hatua za makusudi matatizo ya magonjwa ya moyo, Kiharusi na figo yatakuwa makubwa sana kwenye mkoa huu", amesema Profesa Janabi.


Katika hatua nyingine pia Profesa Mohamed Janabi ameahidi kukutana na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha Dkt. Charles Mkombachepa ili kujadili kwa kina mkakati wa kuchukua, katika udhibiti wa kiwango kikubwa cha shinikizo la juu la damu linalowakabili wananchi wa Mkoa wa Arusha pamoja na Mkoa wa Kilimanjaro.

Daktari huyo bingwa wa Moyo amesema ni muhimu kwa wananchi kuwa makini na lishe akionya kuhusu ulaji wa hovyo wa vyakula pamoja na matumizi makubwa ya pombe ambayo yamekuwa yakigharimu maisha ya watu wengi kutokana na magonjwa yasiyokuwa yakuambukiza ambayo hugharimu fedha nyingi kwenye matibabu.

Shirika la afya duniani WHO linaonya kuwa ulaji wa chumvi usiozingatia vipimo vinavyoshauriwa una madhara makubwa kiafya huku ustaarabu wa kuongeza chumvi mezani ukichochea zaidi madhara hayo kwa watu wengi kote duniani hasa kwenye nchi nyingi zinazoendelea.

Post a Comment

0 Comments