Na John Walter -Babati
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Babati Vijijini Mhe. Daniel Sillo ameshiriki kwenye harambee katika Kanisa la kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mamire Dayosisi ya Kaskazini Kati Jimbo la Babati kwa ajili ya umaliziaji ujenzi wa kanisa hilo.
Katika harambee hiyo jumla ya shilingi milioni 29,541,000 zimepatikana sawa na asilimia 99 ambapo lengo ilikuwa ni kupatikana kwa shilingi Milioni 30,000,000 ili ujenzi huo ukamilike
Sillo akizungumza na waumini wa kanisa hilo leo Septemba 15, 2024 kwenye Ibada iliyofanyika kanisani hapo, alitoa wito kwa waumini kushiriki kikamilifu katika harambee na shughuli nyingine ili kusaidia maendeleo ya kanisa na hata kwenye kijamii.
Aidha Mhe. Sillo alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na makanisa katika kukuza maendeleo ya jamii.
Kwa upande wake Mkuu wa Jimbo la Babati Kanisa la KKKT, Mchungaji Robert Mallya aliwasihi waumini kumtumikia Mungu kwa furaha pamoja na kuijenga nyumba ya ibada kwa moyo wa shangwe na vigelegele. Aliongeza kuwa nyumba nzuri ya ibada ni chanzo cha utukufu na shukrani kwa Mungu.
"Ni muhimu kuja mbele zake kwa shangwe, kwa sababu kujenga nyumba ya Bwana sio tu kazi ya kimwili, bali pia ni ibada ambayo inathibitisha imani yetu na upendo wetu kwake" alisema Mchungaji
Naibu Waziri Sillo aliongozana na Mbunge wa Babati Mjini Mhe. Paulina Gekul katika ibada hiyo iliyofanyika Usharika wa Mamire jimbo la Babati dayosisi ya Kaskazini Kati.
0 Comments