FFU Manyara wapanda miti kanisa la KKKT Singe.

Na John Walter -Babati

Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoa wa Manyara, kimeonesha mshikamano na jamii kwa kushiriki katika zoezi la kutunza mazingira kupitia upandaji miti katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Singe.

Zoezi hilo muhimu limehudhuriwa na askari wa FFU wakiongozwa na Kamanda wa Kikosi hicho, Thomas Mbilinyi, ambaye pia ndiye aliyetoa miche ya miti kwa ajili ya upandaji.

Viongozi wa kanisa waliokuwepo ni Mchungaji wa Usharika wa Singe, Magdalena Khaday, pamoja na Mwinjilisti Kiongozi wa Mtaa wa Singe, Liston Kimambo.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Kamanda Mbilinyi aliwataka waumini wa KKKT na jamii kwa ujumla kuona umuhimu wa kutunza mazingira kwa kupanda miti na kuitunza ili kuepuka madhara yanayotokana na uharibifu wa mazingira kama ukame na mmomonyoko wa udongo.

Kwa upande wake, Mchungaji Magdalena Khaday aliwashukuru askari wa FFU kwa moyo wao wa kujitoa kwa jamii na kushiriki katika juhudi za kuhifadhi mazingira. 

Alisisitiza kuwa kanisa litaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali katika miradi ya kijamii inayolenga maendeleo endelevu.

Mwinjilisti Liston Kimambo naye alisisitiza umuhimu wa jamii kushirikiana na taasisi za serikali katika miradi ya maendeleo, akisema kuwa hatua ya FFU Manyara ni mfano mzuri wa ushirikiano kati ya vyombo vya usalama na jamii kwa ustawi wa mazingira na jamii kwa ujumla.

Zoezi hilo limeacha alama ya mshikamano kati ya Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Kutuliza Ghasia na wananchi wa Singe, Manyara, likiwa sehemu ya jitihada endelevu za utunzaji wa mazingira na ushirikiano wa kijamii.


Picha mbalimbali kikosi cha kutuliza ghasia mkoa wa Manyara wakipanda miti katika kanisa la KKKT mtaa wa Singe.







Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items