Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Mussa Nsekela ametangaza matokeo ya uuzaji wa hatifungani ya Samia Infrastructure Bond ambapo Shilingi Bilioni 323 zimekusanya sawa na 215%, ikiwa ni zaidi ya 115% ya lengo la kukusanya Shilingi Bilioni 150.
Matokeo hayo yametangazwa katika hafla iliyofanyika leo katika hoteli ya Johari Rotana ambapo Mgeni rasmi alikuwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi - TAMISEMI, Mhe. Mohammed Mchengerwa, na kuhudhuriwa na Kamati ya Bunge - TAMISEMI, pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali, pamoja na taasisi za umma na binafsi.
Nsekela ameeleza kuwa mauzo ya shilingi bilioni 323 yanatokana na kampuni na taasisi 327 ambazo zimewekeza zaidi ya shilingi bilioni 118.99 pamoja na watu binafsi 6,896 waliowekeza jumla ya shilingi bilioni 204.1. Asilimia 94 ya uwekezaji umefanyika kidijitali kupitia SimBanking.
Mafanikio haya tuliyoyapata yanadhihirisha imani ya wawekezaji kwa Benki yetu, na uwezo wa Watanzania kufanikisha kukusanya fedha kwa ajili ya kufanikisha miradi ya maendeleo nchini.
Nsekela ameishukuru Serikali kwa fursa ya kipekee ya kusaidia kukusanya fedha kwa ajili ya miundombinu ya barabara zilizochini ya TAMISEMI kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko na Mitaji (CMSA), Cpa Nicodemus Mkama amesema kuorodheshwa kwa Hatifungani ya Miundombinu ya Samia, kumeongeza thamani ya uwekezaji katika Hatifungani za Kampuni na Taasisi kwa asilimia 38.59 na kufikia Shilingi trilioni 1.16, kutoka Shilingi bilioni 837.31. CPA Mkama amesema mafanikio hayo yanaonyesha imani waliyonayo wawekezaji kwa Benki ya CRDB na masoko ya mitaji.
.jpeg)

