F DED BABATI: "Jamii yote inawajibika katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia" | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

DED BABATI: "Jamii yote inawajibika katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia"



Na John Walter -Babati, Manyara

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Shabani Mpendu, amesema kuwa mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia yanahitaji ushiriki wa jamii nzima, huku akitoa wito kwa viongozi wa mitaa na vijiji kuhakikisha ajenda ya ukatili wa kijinsia inakuwa ajenda kuu katika vikao vyote vya maendeleo.

Akizungumza wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha wadau mbalimbali kujadili mbinu za kukomesha vitendo vya ukatili, Mpendu alisema kuwa bado kuna changamoto ya utoaji taarifa juu ya matukio ya ukatili. 

“Kwa muda mrefu jamii imekuwa ikishughulikia matukio haya kifamilia kwa kutumia mila kama fidia ya mbuzi, kondoo au ng’ombe badala ya kuchukua hatua za kisheria,” alisema.

Kwa mujibu wa takwimu zilizowasilishwa, mwaka 2022 kulikuwa na matukio 683 ya ukatili wa kijinsia yaliyoripotiwa, mwaka 2023 yakaongezeka hadi 1,765, mwaka 2024 yakashuka hadi 1,220, na kuanzia Januari hadi Mei 2025 tayari matukio 416 yameripotiwa.

Takwimu hizi zinaonyesha hali ya ukatili bado ni ya kutia wasiwasi.

Katika kikao hicho, Mkurugenzi Mpendu alielekeza kuwa watendaji wa kata, mitaa na vijiji wahakikishe wanafanya vikao vya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu vita dhidi ya ukatili wa kijinsia, pamoja na kuwajengea uelewa wa kisheria na kijamii juu ya madhara ya ukatili huo.

Aidha, kwa mujibu wa taarifa ya Dawati la Jinsia na Watoto ya Polisi Wilaya ya Babati iliyowasilishwa na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Fatuma Silaa, ndani ya miezi mitatu ya kwanza ya mwaka 2025 (Januari hadi Machi), jumla ya matukio 68 ya ukatili wa kijinsia yameripotiwa wilayani humo.


Naye Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum katika Halmashauri ya Mji wa Babati, Ali Mwinyikombo, alisema kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendelea kutoa elimu na kuweka mikakati madhubuti ya kukomesha ukatili huo.


"Tumeazimia kushirikiana kwa karibu kuhakikisha hakuna mwananchi anayebaki nyuma kwenye mapambano haya,” alisema.

Wadau mbalimbali walioshiriki katika kikao hicho wamependekeza kujengwa kwa nyumba salama kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia, pamoja na kuendelea kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuripoti matukio hayo kwa vyombo husika badala ya kuyamaliza kifamilia au kimila.

Kwa sasa, Halmashauri ya Mji wa Babati inashika nafasi ya tatu kimkoa kati ya halmashauri saba za Mkoa wa Manyara kwa kuwa na idadi kubwa ya matukio ya ukatili wa kijinsia yaliyoripotiwa.

Mkutano huo ulihudhuriwa na watendaji wa kata, vijiji, wanasheria, Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia, Magereza na wadau wengine wanaojihusisha na masuala ya haki za binadamu na ustawi wa jamii.

Wadau mbalimbali katika kikao hicho.













Post a Comment

0 Comments