Na John Walter -Babati
Maadhimisho ya Wiki ya Zimamoto Duniani yamefanyika leo mkoani Manyara, yakiongozwa na Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani humo, RFO Gilbert Mvungi.
Maadhimisho hayo yameambatana na shughuli mbalimbali za kijamii na utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu tahadhari na uokoaji katika majanga ya moto.
Kamanda Mvungi ametumia mamlaka aliyopewa kupandisha vyeo baadhi ya maafisa wa jeshi hilo, kuanzia ngazi za chini hadi za kati akieleza kuwa, hatua hiyo inalenga kuongeza motisha kwa askari hao ili waendelee kutoa huduma bora kwa wananchi.
Maafisa wa Zimamoto, wakiwa wamevalia sare zao na kubeba mabango yenye ujumbe wa kaulimbiu ya mwaka huu isemayo "Shujaa wa Moto, Mlinzi wa Maisha: Okoa Maisha na Mali, Piga 114", walipita mitaa mbalimbali ya mji wa Babati wakihamasisha matumizi ya namba hiyo wakati wa dharura.
Kamanda Mvungi ameeleza kuwa elimu wanayoitoa mara kwa mara imeanza kuzaa matunda, kwani wananchi wameanza kuelewa umuhimu wa kutoa taarifa mapema kupitia namba ya bure ya dharura 114.
Amesisitiza umuhimu wa kutumia namba hiyo kwa usahihi na kutoa taarifa kamili kulingana na anuani sahihi ya tukio ili kurahisisha utoaji wa msaada wa haraka.
Aidha, ameishukuru serikali kwa kuendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa jeshi hilo, ikiwa ni pamoja na utoaji wa magari ya kuzimia moto.
Amesema wanatarajia kupokea magari hayo katika kila wilaya ya mkoa huo, hatua itakayoongeza ufanisi wa utendaji kazi wao.
Kwa upande wake, ASF Henry Mwaluseke, akizungumza kwa niaba ya askari wenzake, amesema kupandishwa vyeo ni chachu ya kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi na kwamba jeshi hilo limejipanga vyema kulinda maisha na mali za wananchi wa Manyara.
Maadhimisho hayo, ambayo kilele chake ni Mei 4 kila mwaka, hufanyika duniani kote kuwakumbuka mashujaa wa Zimamoto na Uokoaji waliopoteza maisha mwaka 1999 nchini Australia wakati wakitekeleza majukumu yao ya kazi.
Hadija Mohamed, mkazi wa mtaa wa Oster Bay mjini Babati, amesema Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limekuwa na mchango mkubwa katika jamii, hasa wakati wa matukio ya dharura huku akiwataka waendelee kuongeza juhudi na kufika kwa wakati katika matukio.
Picha mbalimbali maadhimisho ya wiki ya Zimamoto Duniani mkoani Manyara Leo mei 2,2025.picha zote zimepigwa na John Walter.
0 Comments