Na John Walter -Babati
Katika juhudi za kurejesha hadhi na matumizi ya mbegu za asili nchini, Kitengo cha Jinsia na Maendeleo (GAD) cha Idara ya Maendeleo ya Jimbo Katoliki la Mbulu kinatekeleza Mradi Jumuishi wa Maendeleo ya Kilimo na Uchumi (Integrated Rural Development Project – IRDP).
Mradi huo unaolenga kuhamasisha kilimo endelevu, unasisitiza matumizi ya mbegu za asili na kuachana na kilimo cha kemikali ambacho kimekuwa na madhara kiafya na kimazingira.
Kwa upande wake, Winfrida Patrick, Mratibu Msaidizi wa Kitengo cha Jinsia na Maendeleo (GAD), anasisitiza kuwa mradi huo unawalenga zaidi wanawake wakulima, kwa kuwa wao ndiyo walinzi wakuu wa mbegu katika jamii nyingi.
“Tunahamasisha wakulima, hasa wanawake, kuwa na uelewa wa kuhifadhi mbegu zao. Mbegu hizi ni urithi, historia, na msingi wa usalama wa chakula na lishe kwa vizazi vijavyo,” amesema Winfrida.
Katika hatua ya kueneza elimu na kushirikiana uzoefu, GAD kwa kushirikiana na wadau wengine iliandaa mafunzo ya siku mbili mjini Babati yaliyohusisha wakulima kutoka vijiji vya Qatesh (Wilaya ya Mbulu), Ayamango na Qash (Wilaya ya Babati Vijijini), pamoja na maafisa kutoka serikali na sekta binafsi.
Mafunzo hayo yalilenga kujadili mikakati ya kuendeleza matumizi ya mbegu za asili na kupunguza utegemezi wa pembejeo zenye kemikali.
William Hamisy kutoka NPGRC – Kitengo cha Taifa cha Hifadhi ya Nasaba za Mimea, aliangazia changamoto zinazoikumba sekta ya mbegu za asili, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na maisha ya kisasa.
“Watu wanakimbilia tija ya haraka, wakisahau kuwa kilimo cha jadi kilikuwa na mizizi ya afya na hifadhi ya ardhi,” amesema Hamisy.
Paul Chilewa kutoka Mtandao wa Kuendeleza Kilimo Hai Tanzania (TOAM), aliitaka serikali kuzingatia mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia kuhusu bayoanuwai na haki za wakulima.
“Mbegu hizi ni msingi wa uhuru wa chakula, Tanzania imeridhia mikataba kama CBD na ITPGRFA, lakini utekelezaji wake bado uko nyuma, Sera zetu lazima zitambue mchango wa wakulima katika kuhifadhi rasilimali za mimea,” amesema Chilewa.
Aliongeza kuwa kupitia Mpango wa Kitaifa wa Mkakati wa Kilimo Ikolojia Hai (NEOAS) 2023–2030, lengo la pili linaeleza wazi kuwa mbegu za mkulima ni msingi wa kilimo ikolojia, na kwamba zinapaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa ili kusaidia serikali kupunguza utegemezi wa virutubisho vya viwandani.
“Huu ni wakati wa kurudisha hadhi ya mbegu za asili kama chanzo cha virutubisho vya asili na suluhisho la changamoto ya lishe nchini,” amesema.
Afisa Kilimo kutoka kijiji cha Ayamango kata ya Galapo William Mkojela, anasema kuwa mradi huo umekuwa mkombozi kwa wakulima wa maeneo hayo, kwa kusaidia kulinda mbegu za asili, afya za binadamu, na kuhifadhi mazingira.
“Tunarejea kwenye misingi yetu ya jadi ambayo haikuharibu afya wala ardhi, mbegu hizi ni sehemu ya utambulisho wetu,” amesema Mkojela.
Kwa ujumla, juhudi za GAD na washirika wake ni mwanga mpya katika mapambano ya kurejesha mbegu za asili kwenye hadhi yake.
Ni mwito wa kizazi hiki kurejea kwenye urithi wa mababu – urithi wa afya, hifadhi ya mazingira, na usalama wa chakula.
0 Comments