Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Njombe Erasto Mpete amewataka wananchi wa halmashauri hiyo kujitokeza katika maeneo ya miradi yatakayotembelewa na Mwenge wa Uhuru ili waweze kupokea ujumbe mahususi wa Mwenge na kujionea jinsi halmashauri yao inavyotekeleza miradi ya maendeleo.
Akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake Mpete amesema,halmashauri ya mji wa Njombe inatarajia kupokea Mwenge wa Uhuru Mei 8 mwaka huu ukitokea wilayani Ludewa ambapo utatembelea katika kata tano na kumpongeza mkurugenzi wa halmashauri hiyo pamoja na wataalamu kwa maandalizi makubwa ya mapokezi.
"Mwenge wa Uhuru utapita katika kata tano za halamashauri ya mji wa Njombe na utaanza kata ya Luponde kijiji cha Madobole kwa hiyo tunaomba sana wananchi wa Madobole kujitokeza kwa wingi maana yake ndio sehemu ya mapokezi ili kuonyesha kwamba halmashauri ya mji wa Njombe tuko vizuri na baada ya kutoka Madobole Mwenge utakimbizwa kata ya Uwemba katika kijiji cha Ikisa na pale kutakuwa na tukio la kukagua msitu unaoitwa Ilonganjaula na mkimbiza mwenge atakabidhi mizinga ya Nyuki"amesema Mpete
Amesema Mwenge wa Uhuru katika kata ya Mji Mwema utapita katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika kiwanda cha uchakataji na kusafirisha mazao ya Parachichi,Kituo cha Afya ambao huduma ya mionzi itazinduliwa na ugawaji wa vyandarua na bima huku pia katika kata hiyo kikietembelewa kikundi cha ujasiriamali wanaojishughulisha na uchoraji na baada ya hapo Mwenge wa Uhuru utaweza kwenda kuzindua madarasa sita katika shule ya sekondari Mpechi.
Vile vile amesema Mwenge wa Uhuru utatembelea kikundi cha wanawake na Samia wahamasishati wa nishati mbadala na matumizi bora ya nishati mbadala kilichopo Njombe mjini na kisha kuelekea katika kata ya Ramadhani katika chuo shirikishi cha sayansi ya tiba utakapofanyika uzinduzi wa klabu ya kupinga rushwa na kurejea Njombe mjini kwenye eneo la mkesha utakapofanyika uzinduzi wa gari jipya la miradi ya maendeleo.
Aidha amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kufikisha fedha kwa ajili ya miradi kwenye halmashauri hiyo "lakini bila kuacha Chama cha Mapinduzi na Kamati zake za siasa kwa misukumo yao kutukumbusha mara kwenye utekelezaji wa Ilani"
0 Comments