Na John Walter -Babati
Ni kama sinema ya marudio! Baada ya siku chache tu tangu Simba SC waichape Singida Black Stars bao 1-0 kwenye Ligi Kuu ya NBC, timu hizo mbili zinakutana tena kesho, lakini safari hii ni kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho la CRDB – mechi ya kisasi inayosubiriwa kwa hamu kubwa kwenye uwanja wa Tanzanite, Kwaraa mjini Babati.
Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, David Ouma, raia wa Kenya, amesema kikosi chake kimejipanga tofauti safari hii na kwamba wamejifunza makosa yao kutoka kwa mechi ya ligi.
“Tunaiheshimu Simba, lakini mechi ya kesho ni hadithi mpya, tupo tayari kupambana na kuhakikisha tunasonga mbele kwenye michuano hii ya CRDB,” amesema Ouma.
Kwa upande wa Simba, Kocha Msaidizi Selemani Matola amesema ushindi wa mwisho dhidi ya Singida hauwafanyi wabweteke. “Tunatambua ubora wa Singida Black Stars, ni timu yenye nidhamu ya mchezo, lakini tumejipanga kuhakikisha tunaibuka na ushindi mwingine,” amesema Matola.
Nyota wa Simba, Mohamed Hussein maarufu kama "Tshabalala", amesema anajua mchezo utakuwa mgumu lakini wana ari kubwa ya kutetea heshima yao.
“Tunajua haitakuwa rahisi, lakini tumejiandaa kikamilifu,” amesema beki huyo kisiki.
Kwa upande mwingine, mshambuliaji wa Singida Black Stars, Eliuter Mpepo, amesisitiza kuwa wameweka msisitizo mkubwa kwenye safu ya ushambuliaji na wana lengo moja tu – kulipiza kisasi. “Tutapambana kwa dakika zote 90, mashabiki wetu waamini tunarudi tofauti kesho,” amesema Mpepo.
Mashabiki wa soka mkoani Manyara wanatarajia kushuhudia burudani ya hali ya juu huku uwanja wa Tanzanite ukitarajiwa kufurika mashabiki wanaosubiri kuona nani ataibuka kidedea kwenye mechi hii ya kuvutia.
Je, Simba wataendeleza ubabe wao au Singida Black Stars wataandika historia kwa kulipiza kisasi? Majibu yatapatikana kesho, uwanja wa Tanzanite Kwaraa.
0 Comments