Na John Walter -Babati
Timu ya Singida Black Stars imefanikiwa kutinga hatua ya fainali ya michuano ya CRDB Cup baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Simba SC katika mchezo uliopigwa leo kwenye Uwanja wa Tanzanite, Kwaraa, mjini Babati.
Mchezo huo wa kusisimua ulishuhudia Singida ikitawala sehemu kubwa ya kipindi cha pili, huku nyota wao wakionyesha nidhamu ya hali ya juu katika utekelezaji wa mbinu za kiufundi.
Bao la kwanza kwa upande wa Singida lilifungwa na mshambuliaji hatari Jonathan Sowah, kabla ya Emmanuel Keyekeh kupachika mabao mawili yaliyohitimisha ushindi mnono kwa kikosi hicho.
Kwa upande wa Simba, bao la kufutia machozi lilifungwa na Aua.
Akizungumza baada ya mchezo, Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, David Ouma, alisema ushindi huo umetokana na wachezaji wake kufuata maelekezo kwa umakini mkubwa.
"Tumeshinda kwa sababu tumefuata maelekezo tuliyopanga. Kila mchezaji anapewa majukumu yake na tunachoangalia ni matokeo ya mwisho (Outcome)," alisema Ouma.
Emmanuel Keyekeh, aliyefunga mabao mawili na kuonyesha kiwango bora katika eneo la kiungo, alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo.
Kwa upande mwingine, Kocha wa Simba, Fadlu Davids, alisema licha ya timu yake kupoteza mchezo, hiyo si dalili ya kushuka kwa kiwango bali ni sehemu ya matokeo ya mpira wa miguu.
"Mpira una matokeo ya aina tatu, na hizi ni changamoto za kawaida, siwezi kusema mechi hizi tatu tulizocheza ni kikwazo, tunaendelea kujifunza na kusonga mbele," alisema Fadlu.
Singida sasa itakutana na Yanga SC katika fainali ya michuano hiyo, mechi inayosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini.
0 Comments