F Wawili wahukumiwa miaka 20 jela kwa kukutwa na nyara ya serikali. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Wawili wahukumiwa miaka 20 jela kwa kukutwa na nyara ya serikali.



Na John Walter -Babati 

Mahakama ya Wilaya ya Babati leo Mei 20, 2025 imetoa hukumu ya kifungo cha miaka 20 jela kwa wanaume wawili waliopatikana na hatia ya kumuua pundamilia na kumiliki nyara za serikali kinyume cha sheria.

Washtakiwa hao ni Ramadhan Hussein Dodi (39) na Mohamed Bakari Chora (30), wakazi wa Kijiji cha Chubi, Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma. Walipatikana na hatia ya kutenda kosa hilo mnamo Oktoba 25, 2024 katika eneo la Chubi lililopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, Wilaya ya Babati mkoani Manyara.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyosomwa mahakamani, washtakiwa walikamatwa wakiwa na kichwa cha pundamilia, miguu ya pundamilia, mkia mmoja pamoja na ngozi ya mnyama huyo. Nyama ya pundamilia waliokuwa wakimiliki ilikadiriwa kuwa na thamani ya Dola za Kimarekani 1,200, sawa na takribani shilingi milioni 3,204,000 za Kitanzania.

Hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Babati, Mheshimiwa Karimu Mushi (PRM), ambapo wote wawili walitiwa hatiani na kuhukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja.

Makosa hayo ni kwa mujibu wa kifungu cha 86 (1) na (2)(c)(iii) cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori, Sura ya 283 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022, pamoja na Aya ya 14, Kifungu namba 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Kuhujumu Uchumi, Sura ya 200 iliyofanyiwa marejeo mwaka huohuo.

Mwendesha mashtaka wa serikali alikuwa Bw. Rusticus Mahundi, huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na Wakili Simon Shirima.

Ingawa wamepatikana na hatia, washtakiwa wamepewa haki ya kisheria ya kukata rufaa endapo hawajaridhika na uamuzi wa mahakama.

Hukumu hiyo imetajwa kuwa onyo kwa wale wote wanaojihusisha na ujangili na uharibifu wa rasilimali za taifa, hasa wanyamapori walio katika hatari ya kutoweka. 

Post a Comment

0 Comments