F Kambi ya Kuunda Timu ya Mkoa Manyara Yakamilika, Wanafunzi 120 Kuchuana UMITASHUMTA Kitaifa | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Kambi ya Kuunda Timu ya Mkoa Manyara Yakamilika, Wanafunzi 120 Kuchuana UMITASHUMTA Kitaifa



Na John Walter -Manyara

Kambi ya kuunda timu ya Mkoa wa Manyara kwa ajili ya mashindano ya UMITASHUMTA ngazi ya kitaifa imekamilika rasmi, ambapo jumla ya wanafunzi 120 kutoka halmashauri zote za mkoa huo wamechaguliwa kuiwakilisha Manyara katika mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika mkoani Iringa kuanzia tarehe 7 Juni, 2025.

Kambi hiyo ilifanyika mjini Babati katika shule ya Sekondari Singe.

Wanafunzi waliopata nafasi ya kuendelea na mashindano ya kitaifa kwa sasa wanaendelea na kambi ya mazoezi ya siku tatu, kwa lengo la kuwaweka tayari na kuwajengea uwezo wa kushindana katika ngazi ya juu.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha kambi hiyo, Afisa Elimu Mkoa wa Manyara, Bw. Halfan Omary, aliwatia moyo wanafunzi ambao hawakuchaguliwa kwa safari ya kitaifa. Aliwahimiza kutokata tamaa na kuwataka kujiandaa vema kwa msimu wa mashindano wa mwaka 2026/2027.

Katika kambi hiyo iliyodumu kwa wiki moja, Wilaya ya Hanang’ iliibuka mshindi wa jumla baada ya kuonyesha uwezo mkubwa katika michezo mbalimbali.

Michezo iliyoshindaniwa katika kambi hiyo maalum iliyosimamiwa na walimu wa michezo wenye uzoefu ni pamoja na:

Mpira wa miguu (wavulana na wasichana)

Mpira wa wavu (wavulana na wasichana)

Mpira wa mikono (wavulana na wasichana)

Netiboli (wasichana)

Soka maalum kwa wavulana (viziwi)

Mpira wa goli maalum (wenye uoni hafifu)

Riadha za kawaida na riadha maalum

Sanaa za jukwaani

Mashindano ya UMITASHUMTA ni jukwaa muhimu kwa wanafunzi kuonyesha vipaji vyao, kukuza ushindani wa michezo shuleni na kuhamasisha ujumuishaji wa watoto wenye mahitaji maalum. Mkoa wa Manyara una matumaini makubwa ya kufanya vizuri katika mashindano yajayo.



Picha mbalimbali wakati wa mashindano hayo katika uwanja wa shule ya Sekondari Singe. 






















Post a Comment

0 Comments