Na John Walter -Mbulu
Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Sayansi za Afya Haydom, Bathomolayo Madangi, amesema taasisi hiyo imejipanga kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza taaluma ya mionzi nchini, ili kuhakikisha kunakuwepo na idadi ya kutosha ya wataalamu wenye ujuzi.
Amezungumza hayo katika MAHAFALI ya 40 chuoni hapo ambapo jumla ya Wanafunzi 132 wamehitimi taaluma mbalimbali kwa miaka mitatu.
Madangi amesema tayari serikali imepeleka wataalamu 60 kupata mafunzo katika taasisi hiyo, na kwa upande wao, taasisi imepanga kusaidia kusomesha wataalamu 100 zaidi kwa gharama nafuu, huku sehemu ya gharama zikigharamiwa na chuo chenyewe.
Ameeleza kuwa lengo ni kuhakikisha huduma za mionzi zinapatikana kwa ufanisi katika maeneo mbalimbali nchini, hasa kwenye hospitali na vituo vya afya vilivyo pembezoni, na kupunguza uhaba wa wataalamu uliopo kwa sasa.
“Tunashirikiana na serikali kuongeza idadi ya wataalamu wa mionzi kwa kutoa mafunzo bora na ya vitendo, ili baada ya kuhitimu wawe tayari kwenda kuwahudumia wananchi kwa ufanisi,” amesema Madangi.
Taasisi ya Mafunzo ya Sayansi za Afya Haydom imeendelea kuwa chachu ya kuandaa wataalamu wa afya kwenye nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na uuguzi, ukunga, teknolojia ya maabara, pharmacy, afisa tabibu na sasa mionzi, kwa lengo la kuboresha huduma za afya nchini.
