Shule ya Sekondari Emboreet yaomba kufanywa ya Bweni kutokana na changamoto ya Wanyama Wakali


Na John Walter -Simanjiro

Uongozi wa Shule ya Sekondari Emboreet, wilayani Simanjiro, umeiomba Serikali kuisajili shule hiyo kuwa ya bweni badala ya kutwa, ili kuwawezesha wanafunzi kuendelea na masomo bila kuhatarisha usalama wao.

Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Aziza Msengesi, akizungumza leo Agosti 23, 2025, amesema umbali mrefu kutoka makazi ya wananchi hadi shuleni na uwepo wa wanyama wakali kama simba, tembo na fisi kumesababisha wanafunzi wengi kushindwa kuripoti.

Ameeleza kuwa mwaka wa masomo 2025, wanafunzi 331 walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza, lakini walioripoti ni 176 pekee huku 155 wakihamishiwa shule nyingine. Aidha, mwaka 2024, waliopangiwa walikuwa 237 lakini walioripoti ni 100 tu kutokana na changamoto hizo.

“Jiografia ya kata ilivyo, baadhi ya vitongoji viko mbali mno. Mfano, kitongoji cha Lemooti kiko kilomita 30 kutoka shuleni, jambo linalowawia vigumu watoto kuja shule kila siku,” alisema Mwalimu Msengesi.

Aliongeza kuwa wazazi wengi wanashindwa kumudu gharama za chakula kwa ajili ya hosteli, hali inayosababisha utoro wa mara kwa mara na hatimaye mdondoko wa wanafunzi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shule, Raymond ole Kisiando, ameunga mkono ombi hilo akisema kuwa bweni ndilo suluhisho pekee litakalopunguza tatizo la wanafunzi kuhama au kukatishwa masomo.

Akijibu changamoto hizo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, aliyefanya ziara shuleni hapo, amesema Serikali imejipanga kusogeza huduma za elimu karibu na wananchi ili kuondoa changamoto za usafiri na usalama.

“Hatupendi watoto watembee kilomita 30 kila siku halafu wakutane na wanyama wakali, hili ni eneo lililo karibu na hifadhi ya wanyama, hivyo ni lazima tupate suluhisho, nimeagiza mkurugenzi wa halmashauri kuwasilisha maombi wizarani ili shule hii isajiliwe kuwa ya bweni,” alisema Profesa Mkenda.

Waziri huyo alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha watoto wanapata elimu katika mazingira salama bila vikwazo vinavyoweza kuhatarisha maisha yao na kupelekea kuporomoka kwa kiwango cha elimu.

Shule ya Sekondari Emboreet iiyojengwa na shirika la ECLAT Foundation chini ya Mwenyekiti Peter Toima (Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Manyara) kwa kushirikiana na shirika la UPENDO association la nchini ujerumani, ina Wanafunzi 962 wa kidato cha kwanza hadi cha sita. 


Picha mbalimbali wakati wa ziara ya Waziri wa Elimu sayansi na teknolojia Profesa Adolf Mkenda shule ya Sekondari Emboreet wilayani Simanjiro mkoani Manyara, picha zote zimepigwa na Mwandishi wetu John Walter






























Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items