F Binti Aliyepotezana na Wazazi Miaka 9 Akabidhiwa Rasmi kwa Familia Yake Babati | Muungwana BLOG

Binti Aliyepotezana na Wazazi Miaka 9 Akabidhiwa Rasmi kwa Familia Yake Babati



Na John Walter-Babati

Viongozi wa Smaujata Wilaya ya Babati wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Shujaa Petro Martini, wamefanikisha zoezi la kumkabidhi kwa wazazi wake msichana aliyepotezana na familia yake kwa muda wa miaka tisa.

Msichana huyo, Mariamu Selemani Ramadhani, aliondoka nyumbani kwao katika kijiji cha Endadosh, kata ya Galapo, Wilaya ya Babati akiwa na umri wa miaka 13 kwenda kufanya kazi za ndani mkoani Kilimanjaro. 

Tangu wakati huo hakuwahi kuwasiliana na wazazi wake, hali iliyosababisha familia yake kudhani kuwa amepotea kabisa.

Akiwa Kilimanjaro, Mariamu alikumbana na changamoto kubwa za maisha ikiwemo kunyanyaswa na kufanyiwa vitendo vya ukatili na mwajiri wake.

Hata hivyo, kwa juhudi za viongozi wa Smaujata mkoa wa Kilimanjaro wakiongozwa na Stella, walibaini hali hiyo na kufanikisha kumwokoa. 

Mwajiri wake alikubali kumruhusu kurudi nyumbani na pia kumlipa fidia ya shilingi milioni 3.4 kwa kazi alizofanya kwa kipindi cha miaka tisa. 

Hata hivyo, amepunguza shilingi milioni moja na kuahidi kulipa kiasi kilichobaki hivi karibuni.

Katika hafla ya makabidhiano, Katibu wa Smaujata Kanda ya Kaskazini, Shujaa Ezekiel Tlanka, amewashukuru viongozi wa Smaujata mikoa ya Kilimanjaro na Manyara kwa ushirikiano wao katika kufanikisha tukio hilo. 

Aidha, ameishukuru Kamati za Ulinzi na Usalama za wilaya za Moshi na Babati, hususan Jeshi la Polisi, kwa msaada wao wa karibu kwa Jumuiya ya Smaujata.

Smaujata kupitia taarifa hiyo imeendelea kutoa wito kwa jamii kuacha tabia ya unyanyasaji kwa wasichana na wanawake, ikisisitiza kuwa vitendo hivyo ni kinyume cha haki za binadamu na havikubaliki katika jamii.

Kwa upande wake, Mariamu aliwashukuru viongozi wa Smaujata mikoa ya Kilimanjaro na Manyara kwa kumsaidia kurejea nyumbani na kumpatanisha na wazazi wake baada ya miaka mingi ya mateso. 

Mama yake pia alishukuru kwa msaada huo, akieleza kuwa aliwahi kukata tamaa na kudhani kuwa binti yake amefariki dunia.

Post a Comment

0 Comments