Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imetoa taarifa ya hali ya masoko ya mitaji nchini Tanzania wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa mauzo ya hatifungani ya ''Stawi Bond'', iliyotolewa na Benki ya TCB leo Septemba 17, 2025 katika Ukumbi wa Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam
Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, CPA. Nicodemus Mkama, alisema kuwa masoko ya mitaji nchini yameendelea kuwa salama, thabiti na bunifu huku yakitoa fursa mbalimbali kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Alibainisha kuwa kati ya Agosti 2021 hadi Agosti 2025, thamani ya uwekezaji katika masoko hayo imeongezeka kwa asilimia 75.25 kutoka shilingi trilioni 31.64 hadi kufikia trilioni 55.45.
“Mafanikio haya ni matokeo ya utekelezaji mzuri wa sera, sheria na miongozo ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema CPA Mkama.
Hatifungani ya Stawi, ambayo imepitia mchakato wa mapitio ya kisheria na kupata idhini rasmi ya CMSA, inalenga kukusanya rasilimali fedha kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs) kukuza biashara zao. Utoaji wa hatifungani hiyo umezingatia Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (Sura ya 79) pamoja na Miongozo ya mwaka 2019 kuhusu utoaji wa hatifungani kwa umma.
Kwa mujibu wa TCB, fedha zitakazopatikana kupitia hatifungani hii zitaelekezwa kwa kampuni zinazomilikiwa na Watanzania, huku wananchi wanaowekeza wakinufaika kwa kulipwa riba. Jambo hili linaendana na malengo ya Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha (FSDMP) 2020/21–2029/30 na Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.
Hatifungani ya Stawi imeweka historia kwa kuwa ya kwanza kutolewa na benki inayomilikiwa na Serikali, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Njia Mbadala za Kugharamia Miradi ya Maendeleo (Alternative Project Financing Strategy). Mkakati huu unalenga kuziwezesha taasisi za umma kupata fedha kupitia masoko ya mitaji badala ya kutegemea fedha kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali.
Kupitia mauzo ya hatifungani hiyo, Benki ya TCB inatarajia kuongeza ukwasi, kuimarisha mtaji na kuboresha huduma kwa wananchi, wajasiriamali na sekta binafsi kwa ujumla. Aidha, benki hiyo inalenga kuongeza ubunifu katika huduma za kifedha kwa kuzingatia mahitaji halisi ya soko.
CMSA imesisitiza kuwa itaendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji kwa kutekeleza mikakati ya kukuza masoko ya mitaji kwa mujibu wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, yenye lengo la kujenga uchumi jumuishi, shindani na endelevu kwa Watanzania wote.
Aidha CMSA CPA. Mkama alikabidhi rasmi idhini ya mauzo ya hatifungani kwa Benki ya TCB, ikiwa ni uthibitisho kwamba bidhaa hiyo mpya ya kifedha imetimiza matakwa yote ya kisheria, kanuni na miongozo ya masoko ya mitaji nchini.
0 Comments