Na John Walter-Manyara
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara, Ndg. Peter Toima, ametangaza rasmi maandalizi ya ujio wa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye anatarajiwa kufanya ziara ya kampeni mkoani humo Oktoba 3, 2025.
Akizungumza katika kikao cha maandalizi kilichofanyika wilayani Hanang’, Toima amesema mkoa uko tayari kumpokea Dkt. Samia, akibainisha kuwa mikakati na maandalizi yote yanakwenda vizuri.
Katika ratiba ya ziara hiyo, Rais Samia atafanya mikutano na kusalimiana na wananchi katika maeneo kadhaa ikiwemo:
✅ Magugu – kusalimiana na wananchi
✅ Katesh – mkutano wa hadhara
✅ Babati Mjini – mkutano wa hadhara katika Stendi ya zamani.
Mwenyekiti Toima amewataka wananchi wa Manyara kujitokeza kwa wingi kumpokea na kumsikiliza mgombea wao, akisisitiza kuwa ujio huo ni fursa ya kipekee kwa wananchi kusikia dira na ahadi za maendeleo kutoka kwa kiongozi huyo wa taifa.
“Kama mkoa tumejipanga vizuri, nawaomba wananchi wa Manyara wajitokeze kwa hamasa kubwa, tumpe heshima na tumuunge mkono mgombea wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Toima.
Ziara ya Dkt. Samia inatarajiwa kuibua msisimko mkubwa wa kisiasa Manyara, huku wengi wakitarajiwa kuhudhuria kwa wingi wakitarajia majibu mazuri kuhusu soko la mbaazi ambalo limekuwa likilalamikiwa na wakulima wengi.
Aidha ziara hiyo muhimu ni ya kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
0 Comments