F SMAUJATA wafuatilia watoto waliokatisha masomo kisa adhabu kali shuleni. | Muungwana BLOG

SMAUJATA wafuatilia watoto waliokatisha masomo kisa adhabu kali shuleni.



Na John Walter-Babati

Viongozi wa SMAUJATA Wilaya ya Babati, wakiwa wameambatana na Katibu wa SMAUJATA Kanda ya Kaskazini, Shujaa Ezekiel Tlanka, wamefika nyumbani kwa watoto waliokatisha masomo kwa muda mrefu ili kubaini sababu zilizowafanya waachane na shule.

Watoto hao walizungumza kwa uchungu mkubwa huku wengine wakitokwa na machozi, wakieleza kuwa walikata tamaa ya shule kutokana na adhabu kali wanazopata mara kwa mara kutoka kwa walimu wao.

Mwanafunzi wa kwanza mwenye umri wa miaka 15 aliyekuwa kidato cha kwanza, amesema alishindwa kuendelea na masomo baada ya kuchapwa viboko vingi mara kwa mara. 

Amefafanua kuwa mara nyingi akikosea somo la mwalimu mmoja, walimu wanne walishirikiana kumchapa viboko vitatu kila mmoja, na kufanya jumla ya viboko 12 kwa kosa moja.

“Wakati mwingine tunapewa adhabu ya kudeki ofisi ya walimu tukiwa wanne, lakini kuna siku tunadeki wawili tu. Nikijaribu kuzungumza na walimu kuhusu ugumu wa adhabu hizi, majibu ni viboko tena. Na mimi ni msichana, je, inaruhusiwa kuchapwa mapajani? Kwa nini tufanyiwe hivyo?” alihoji Binti huyo huku akilia.

Ameongeza kuwa aliacha shule tangu mwezi Mei na yuko tayari kurejea shuleni iwapo adhabu hizo kali zitaondolewa.

Kwa upande wake, kijana wa kiume mwenye umri wa miaka 17 aliyekuwa kidato cha pili, amesema aliacha shule tangu mwezi Februari kwa sababu ya viboko. 

Ameeleza kuwa mwaka huu alitarajia kufanya mtihani wa kidato cha pili, lakini alishindwa kutokana na kukatisha masomo. “Ninapokumbuka adhabu hizo nakata tamaa ya shule, ila niko tayari kurudia darasa iwapo adhabu kali hazitatolewa tena,” alisema.

Watoto hao wameonyesha uwezo wao wa kitaaluma ambapo binti alikuwa na wastani wa darasa la saba wa alama C na mvulana alipata wastani wa B.

Mwenyekiti wa mtaa Ayabadiney kata ya Bonga wilaya ya Babati mjinim Omari Shabani amewashukuru viongozi wa SMAUJATA kwa kufika hadi nyumbani kwa watoto hao na kuwapa moyo wa kurejea shuleni.

“Watoto hawa ni wajukuu wangu, tulijaribu kuwasihi warudi shule lakini walikataa, hata hivyo, kwa ujio wenu, wamekubali kuendelea na masomo baada ya kupata elimu ya faida ya shule. 

Tunaomba serikali iangalie upya aina ya adhabu zinazotolewa mashuleni, maana watoto wengi wanakimbia shule kwa sababu hiyo,” alisema.

Aidha, wazazi wa watoto hao wametoa shukrani zao kwa SMAUJATA na kuwatakia baraka viongozi wa SMAUJATA.

Kwa upande wake, Katibu wa SMAUJATA Kanda ya Kaskazini, Shujaa Ezekiel Tlanka, amewapongeza viongozi wa Wilaya ya Babati kwa kuibua tukio hilo na kuahidi kwamba SMAUJATA itaendelea kupambana na matukio yote ya ukatili bila kujali nani anafanyiwa.

Amesema wamekubaliana kwamba Jumatatu ijayo watasindikiza watoto hao kurudi shuleni kwa kushirikiana na Ofisi ya Maendeleo ya Jamii pamoja na Dawati la msaada wa kisheria wa Mama Samia, ili kuhakikisha wanaendelea na masomo yao bila uonevu wala manyanyaso.

Post a Comment

0 Comments