Na Ahmad Mmow, Lindi.
Jeshi la Polisi mkoani wa Lindi linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kukutwa na miundombinu ya kujengea madaraja(scaffolds) 511 pamoja na rimu ya tairi ya gari kubwa (lori) kinyume cha sheria.
Watuhumiwa hao walikamatwa tarehe 16 Septemba 2025 majira ya saa nne asubuhi, kufuatia taarifa kutoka kwa raia wema waliohusika kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola.
Kwamujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa( RPC) wa Lindi, Kamishna Msaidizi wa Polisi(ACP) John Imori, miundombinu hiyo ilikamatwa katika stoo ya mmoja wa watuhumiwa, ambaye tayari alikuwa ameipakia kwa ajili ya kusafirishwa kuelekea Dar es Salaam.
Alisema tukio hilo ni mfano wa mafanikio yanayotokana na ushirikiano wa karibu baina ya wananchi na Jeshi la Polisi katika kukabiliana na uhalifu.
Kamanda Imori aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Ibrahimu Hamisi Mkunga (54), Antony Vitus Mtisa (41), Maino Mohamed Selemani (43), Bakiri Kassim Mkunga (45), na Mwinyi Mohamed Pongwa (21), wote wakazi wa eneo la Njia Nne, wilaya ya Kilwa.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa katika msako maalumu uliofanyika kufuatia taarifa zilizopokelewa mapema asubuhi hiyo.
Alisema, mara baada ya taratibu za awali za upelelezi kukamilika, watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili.
Kamanda huyo wa polisi wa mkoa wa Lindi ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa kuhusu vitendo vya uhalifu ili kusaidia kudumisha amani na usalama katika jamii.
0 Comments