Wadau wa maendeleo, wasomi na wataalamu kutoka sekta binafsi na uma wamesema Tanzania imepiga hatua kupitia Dira 2025 licha ya changamoto za kiuchumi za kimataifa huku wakitaja kuwa kilimo bado ni sekta dhaifu kutokana na utegemezi wa mvua na ukosefu wa viwanda vya zana za kilimo na kushauri kuongezwa uwekezaji katika umwagiliaji, miundombinu ya uchumi na ushiriki wa vijana.
Mijadala hiyo imeibuka katika Kongamano la uchumi Jumuishi lililofanyika wiki hii Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Kigoda cha Profesa cha Mwalimu Julius K. Nyerere, kwa kushirikiana na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC) huku baadhi wakisisitiza umuhimu wa kujenga uchumi jumuishi unaozigusa moja kwamoja jamii.
Mwenyekiti wa kongamano hilo, Profesa Alexander Makulilo amebainisha kuwa Kongamano hilo lenye lengo la kusisimua viashiria vya ujenzi na ukuaji wa uchumi linakuja muda mfupi baada Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kuzindua Dira ya 2050 mnamo Julai 17, 2025, na kusisitiza kuwa kila Mtanzania ana wajibu wa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wake.
Akitoa maelezo kuhusu dira hiyo, Ndugu Jordani Matonya ameeleza kuwa dira ya maendeleo imejengwa juu ya misingi ya utawala bora, usalama, amani na utulivu na kusisitiza kuwa nguzo kuu tatu za dira ni uchumi jumuishi na imara, maendeleo ya watu, na uhifadhi wa mazingira, huku akitaja sekta za mageuzi zitakazowezesha utekelezaji wake kuwa ni kilimo cha umwagiliaji, utalii, viwanda na huduma za kifedha.
Mkurugenzi mkuu wa kituo cha ubia PPP David Kafulila ameeleza nafasi muhimu ya ubia kati ya serikali na sekta binafsi katika kufanikisha maendeleo ya Taifa akisema miradi mikubwa kama bandari, barabara na majengo imefanikiwa kupitia ushirikiano huo, hivyo sekta binafsi ni nguzo kuu ya kufanikisha Dira 2050.
Washiriki wengine walihimiza kila Mtanzania kushiriki na kunufaika na dira hiyo kwa kutumia teknolojia, mabadiliko ya mitazamo na mshikamano wa karibu kati ya sekta zote.
0 Comments