Wananchi wa vijiji 10 vinavyozunguka Hifadhi ya Wanyamapori Burunge (JUHIBU) wametakiwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kuhifadhi wanyamapori kwa ajili ya maendeleo ya vijiji vyao.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Burunge (JUHIBU), Patricia Mosea, wakati akiwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya darasa la saba katika Shule ya Msingi Mbugwe, kata ya Mwada wilayani Babati, mkoani Manyara.
Shule ya Msingi Mbugwe, iliyoanzishwa mwaka 1947 na kutambulika kama moja ya shule kongwe mkoani Manyara, ilifanya mahafali yake ambapo jumla ya wanafunzi 83 walihitimu kati ya wanafunzi 122 waliokuwa wameanza darasa la kwanza. Kati yao, wavulana ni 46 na wasichana 37.
Katika risala yao, wanafunzi walieleza changamoto zilizowakabili ikiwemo baadhi ya wenzao kuacha shule kutokana na shughuli za kiuchumi zinazofanywa na wazazi wao, hususan kilimo na ufugaji, hali iliyowakwamisha kutimiza ndoto zao.
Pia wametaja changamoto ya gharama za uendeshaji wa mitihani inayohitaji zaidi ya shilingi milioni 16 kila mwaka.
Akizungumza na wazazi, Mosea aliwataka kuhakikisha watoto wao wanasoma badala ya kuwashirikisha kwenye shughuli za kiuchumi, akisisitiza kuwa elimu ndiyo njia pekee ya kuwatoa watoto katika changamoto za kimaisha.
“Wazazi watimize wajibu wao wa malezi na kuhakikisha watoto wanapata nafasi ya kusoma bila vikwazo,” alisema.
Aidha, amewataka wanafunzi kuwa na nidhamu, kuwatii wazazi na kujituma katika masomo yao.
Amesisitiza kuwa baada ya kuhitimu, watoto wasipoteze muda katika matembezi ya kifamilia bali waendelee na masomo ya ziada ili kujiandaa vyema kwa hatua zinazofuata.
Kuhusu changamoto ya mitihani, Mosea ametangaza kuwa JUHIBU itachangia shilingi milioni moja kusaidia gharama za uendeshaji wa mitihani katika shule hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwada, Laurent William, amesema kijiji kitaendelea kushirikiana na JUHIBU katika kulinda wanyamapori kwa kuzingatia kauli mbiu yao isemayo “Tembo kwa Maendeleo”.
Aidha, ameahidi kuwa kijiji kitachangia gharama za steshenari na mahindi kilo 52 kwa kila mwanafunzi wa kijiji hicho atakayejiunga na kidato cha kwanza.
0 Comments