F Msichana aliyefanyiwa ukatili Kilimanjaro afariki dunia | Muungwana BLOG

Msichana aliyefanyiwa ukatili Kilimanjaro afariki dunia


Na John Walter, Babati

Msichana Mariamu Selemani Ramadhani, mkazi wa kijiji cha Endadosh, kata ya Galapo wilayani Babati, mkoa wa Manyara, amefariki dunia baada ya kupitia mateso na vitendo vya ukatili alipokuwa akifanya kazi za ndani mkoani Kilimanjaro.

Mariamu aliondoka nyumbani kwao akiwa na umri wa miaka 13 kwenda kutafuta maisha kama mfanyakazi wa ndani, lakini tangu kuondoka hakuwahi kuwasiliana na wazazi wake, jambo lililowafanya waamini kuwa amepotea kabisa.

Akiwa mkoani Kilimanjaro, Mariamu alikumbana na mateso makubwa na vitendo vya kinyama kutoka kwa mwajiri wake. 

Baada ya muda, viongozi wa Jumuiya ya Smaujata mkoa wa Kilimanjaro, wakiongozwa na Stella, waligundua hali hiyo na kufanikisha kumwokoa kutoka mikononi mwa watesi wake.

Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa hata siku aliyokabidhiwa kwa ndugu zake, Mariamu alikuwa anaumwa, na hali yake iliendelea kudhoofika hadi kufariki dunia.

Jana, Jumuiya ya Smaujata ilishiriki katika mazishi yake yaliyofanyika kitongoji cha Maweni, kijiji cha Endadosh, kata ya Qash wilayani Babati. 

Viongozi hao waliongozana na Katibu wa Smaujata Kanda ya Kaskazini, Shujaa Ezekiel Tlanka, ambaye alitoa wito kwa jamii kuwalinda watoto dhidi ya unyonyaji na ajira za utotoni.

Akizungumza kwa niaba ya Jumuiya hiyo, viongozi wa Smaujata waliwakumbusha wazazi kuwa ni kosa kubwa kuruhusu watoto wenye umri mdogo kuacha shule na kwenda kufanya kazi majumbani kwa watu kwa lengo la kujipatia kipato.

“Mzazi mtoto anaondoka nyumbani, hatoi taarifa kwa serikali, wala hafuatilii. Ni wajibu wetu sote kuhakikisha ulinzi wa mtoto unaanza nyumbani,” walisema viongozi wa Smaujata.

Kifo cha Mariamu kimeacha simanzi kubwa kwa familia, majirani na watetezi wa haki za watoto, huku wito ukitolewa kwa jamii kushirikiana na mamlaka kuhakikisha visa vya aina hii havijirudii tena.

Post a Comment

0 Comments