F Mulokozi amlilia Raila Odinga. | Muungwana BLOG

Mulokozi amlilia Raila Odinga.

Na John Walter-Manyara

Mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania, David Mulokozi, ameungana na maelfu ya waombolezaji barani Afrika kuomboleza kifo cha aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Amolo Odinga, aliyefariki dunia akiwa nchini India.

Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Mulokozi ameonyesha huzuni yake kwa kuandika ujumbe wa kugusa mioyo, akiambatanisha na picha yake akiwa na marehemu Odinga.

“Pumzika kwa amani, mzee wetu Raila Odinga (Baba). Mwendo wako umeumaliza, lakini urithi wako wa uongozi, mapambano na upendo utadumu milele mioyoni mwa watu,” aliandika Mulokozi.

Ameongeza kuwa Raila Odinga hakuwa tu mwanasiasa bali pia mshauri na kielelezo cha uadilifu hata kwa jamii ya wafanyabiashara, akisisitiza kuwa alikuwa akitoa mafunzo ya kujituma, kujiamini na kufanya mambo kwa heshima.

“Sio siasa tu, bali hata jamii ya wafanyabiashara umekuwa ukitushauri mengi ya msingi na uadilifu, ukitufundisha thamani ya kujiamini, kushikamana na kufanya mambo kwa heshima,” alisema.

Mulokozi amehitimisha kwa kusema kuwa mchango wa Raila Odinga katika uongozi na maendeleo ya Afrika utaendelea kukumbukwa kwa vizazi vijavyo.

“Roho yako ipumzike kwa amani,” ameandika kwa uchungu.

Kifo cha Raila Odinga kimezua majonzi makubwa katika eneo la Afrika Mashariki, ambapo viongozi mbalimbali wameendelea kutuma salamu za rambirambi wakimtaja kuwa nguzo ya demokrasia na haki za wananchi.



Post a Comment

0 Comments