F Bajuta ahitimisha kampeni, awaomba wananchi wa Ufana wajitokeze kupiga kura za CCM. | Muungwana BLOG

Bajuta ahitimisha kampeni, awaomba wananchi wa Ufana wajitokeze kupiga kura za CCM.



Na John Walter -Babati

Mgombea udiwani wa Kata ya Ufana, Jimbo la Babati VijijiniBernard Bajuta amehitimisha rasmi kampeni zake za siku 60 kwa kuwataka wananchi wa kata hiyo kujitokeza kwa wingi kesho, Oktoba 29, kupiga kura na kukichagua Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza katika mkutano wa kufunga kampeni uliofanyika kijijini Ufana, Bajuta amesema kipindi chote cha kampeni amepata nafasi ya kuwasilisha kwa wananchi utekelezaji wa Ilani ya CCM 2025–2030, ambayo imejaa mikakati ya kuwaletea maendeleo endelevu wananchi wa vijiji na vitongoji vyote vya kata hiyo.

Ameeleza kuwa CCM imethibitisha kwa vitendo kuwa ni chama kinachotekeleza ahadi zake kupitia miradi ya maji, umeme vijijini, barabara na kuboresha huduma za afya na elimu, hivyo wananchi hawana sababu ya kupoteza kura zao kwa vyama visivyo na dira ya maendeleo.

“Nawaomba wananchi wote wa Ufana, kesho asubuhi mapema mjitokeze kwa wingi kwenye vituo vyenu vya kupigia kura. Tuwe wa kwanza kupiga kura za ushindi kwa CCM, chama pekee kinachoendelea kuwaletea Watanzania maendeleo ya kweli,” amesema Bajuta.

Aidha, amewashukuru viongozi wa chama, makada, na wafuasi wa CCM kwa ushirikiano waliompa kipindi chote cha kampeni, akiahidi kuwa akipewa ridhaa ataendelea kushirikiana nao katika kuleta maendeleo ya kata ya Ufana.

Kata ya Ufana ni miongoni mwa kata zinazounda Jimbo la Babati Vijijini, ambapo wananchi wanatarajia kupiga kura kesho kuchagua Rais, Mbunge na Madiwani kote nchini.


Chapisha Maoni

0 Maoni