F DC Fakii akagua vifaa tiba hospitali ya wilaya Simanjiro. | Muungwana BLOG

DC Fakii akagua vifaa tiba hospitali ya wilaya Simanjiro.


Na John Walter-Manyara

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Mheshimiwa Fakii Lulandala, amefanya ziara ya kutembelea na kukagua vifaa tiba vilivyopo katika Hospitali ya Wilaya ya Simanjiro, kwa lengo la kujionea hali ya utoaji wa huduma za afya na matumizi ya vifaa vya kisasa vilivyofikishwa hospitalini hapo.

Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Lulandala aliambatana na baadhi ya wataalamu wa Halmashauri pamoja na Maafisa Tarafa, ambapo walipata fursa ya kutembelea na kujionea vifaa tiba vya kisasa vyenye hadhi ya hospitali za kitaifa.

Miongoni mwa vifaa hivyo ni vifaa vya mionzi, vifaa vya kuhifadhia watoto waliozaliwa njiti, mashine za macho za kidigitali, pamoja na mashine za kisasa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), ambavyo havikuwahi kuwepo katika hospitali hiyo miaka ya nyuma.

Mheshimiwa Lulandala ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada kubwa ilizofanya katika kuimarisha sekta ya afya.

Amesema kuwa kwa mara ya kwanza hospitali hiyo imefanikiwa kupata vifaa tiba vya kiwango cha juu ambavyo vimekuwa msaada mkubwa kwa jamii, kwani huduma nyingi za matibabu sasa zinapatikana ndani ya Wilaya ya Simanjiro, hali inayowapunguzia wananchi gharama na usumbufu wa kufuata huduma umbali mrefu.

Aidha, Mheshimiwa Lulandala ameeleza kuwa hadi sasa, sekta ya afya haina deni kwa Serikali ya Awamu ya Sita, kwani imefanya juhudi kubwa kuimarisha miundombinu ya afya kwa ujumla, ikiwemo ujenzi wa majengo, upatikanaji wa vifaa tiba pamoja na ajira za watumishi wa afya kwa wingi.

Kutokana na mafanikio hayo, amewasihi watumishi wa hospitali hiyo kuendelea kuzingatia uchapakazi, maadili ya taaluma na matumizi ya lugha nzuri kwa wagonjwa, ili kuendana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Simanjiro, Sebaldi Mtitu, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwekeza fedha nyingi katika kuboresha miundombinu ya afya pamoja na rasilimali watu.

Ameahidi kusimamia majukumu yake kwa kuzingatia misingi, sheria na kanuni za kazi za kitaaluma, ili kuendelea kuijengea Serikali imani kwa wananchi kuhusu upatikanaji wa huduma bora za afya katika hospitali za Serikali.


Picha mbalimbali za vifaa tiba hospitali ya wilaya ya Simanjiro.





 

Chapisha Maoni

0 Maoni