F Mbunge wa viti maalum (wafanyakazi) Halima Idd Nassor afariki dunia | Muungwana BLOG

Mbunge wa viti maalum (wafanyakazi) Halima Idd Nassor afariki dunia


Na John Walter-Dar es Salaam

Mbunge wa Viti Maalum (Wafanyakazi), Mheshimiwa Halima Idd Nassor, amefariki dunia leo Jumapili tarehe 18 Januari, 2026 akiwa anapatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), jijini Dar es Salaam.

Taarifa za kifo chake zimethibitishwa rasmi na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu, ambaye amesema:
“Kwa masikitiko makubwa, natangaza kifo cha Mbunge wa Viti Maalum, Mheshimiwa Halima Idd Nassor, kilichotokea leo tarehe 18 Januari, 2026 jijini Dar es Salaam. Katika kipindi hiki kigumu…”

Spika ameongeza kuwa Ofisi ya Bunge, kwa kushirikiana na familia ya marehemu, inaendelea kuratibu mipango ya mazishi na kwamba taarifa zaidi zitaendelea kutolewa kwa umma kadri mipango inavyokamilika.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Bunge, mazishi ya marehemu Mheshimiwa Halima Idd Nassor yatafanyika leo Jumapili tarehe 18 Januari, 2026 saa 10 jioni, katika Makaburi ya Kibada kwa Dole, Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

Msiba upo nyumbani kwa marehemu Kigamboni, Dar es Salaam, ambapo ndugu, jamaa, marafiki pamoja na viongozi mbalimbali wanaendelea kutoa pole kwa familia.

Kifo cha Mheshimiwa Halima Idd Nassor ni pigo kubwa kwa familia, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na taifa kwa ujumla, kutokana na mchango wake katika kuwatumikia wafanyakazi na wananchi kwa ujumla. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.

Chapisha Maoni

0 Maoni