Na John Walter-Manyara
Serikali imeanza rasmi utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote (BAW) kuanzia Januari 26, 2026, siku chache baada ya kuzinduliwa kitaifa Januari 23, 2026, ikiwa ni hatua muhimu katika kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya kwa uhakika bila vikwazo vya kifedha.
Mkoani Manyara, Mkuu wa Mkoa Mheshimiwa Queen Sendiga ameonesha dhamira ya dhati katika utekelezaji wa mpango huo kwa kuwa mstari wa mbele kutoa elimu kwa wananchi wa Mji wa Babati.
Kupitia ziara za nyumba kwa nyumba na kutembelea mitaa mbalimbali, Mkuu wa Mkoa amekuwa akitoa ufafanuzi wa kina kuhusu faida, taratibu na umuhimu wa kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote.
Katika ziara hizo, Mheshimiwa Sendiga amekutana na makundi mbalimbali ya wananchi yakiwemo vijana wa bodaboda na bajaji, wazee katika vijiwe pamoja na kaya tofauti, ambapo amesisitiza kuwa bima ya afya ni kinga muhimu dhidi ya gharama kubwa za matibabu na ni nyenzo ya kumuwezesha mwananchi kupata huduma kwa wakati.
Wananchi waliopata fursa ya kuzungumza na Mkuu wa Mkoa waliuliza maswali mbalimbali na kupatiwa majibu, jambo lililosababisha mwitikio chanya na kuongezeka kwa uelewa kuhusu mpango huo.
Wengi wao wameonesha kuunga mkono jitihada za Serikali, huku wakiitaka kuhakikisha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote unaambatana na uboreshaji wa huduma katika vituo vya afya na hospitali ili bima hiyo iwe na tija kwa walengwa.
Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote umeanza kutekelezwa kwa awamu ya kwanza, ukilenga makundi maalum yasiyo na uwezo yakiwemo wazee, watoto, wajawazito na watu wenye ulemavu.
Kwa makundi hayo, gharama za matibabu zitagharamiwa na Serikali, hatua inayolenga kupunguza mzigo wa gharama za afya kwa wananchi walio katika mazingira magumu.
Kwa mujibu wa Serikali, Kitita cha Huduma Muhimu kwa awamu ya kwanza kimeanza kutumika rasmi Januari 26, 2026, kikihusisha wananchi wanaogharamiwa na Serikali.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, alisema gharama ya kitita hicho ni shilingi 150,000 kwa mwaka kwa kaya isiyozidi watu sita.
Waziri Mchengerwa aliongeza kuwa huduma za matibabu zitatolewa kwa kuzingatia utaratibu wa rufaa katika vituo vya afya na hospitali zilizoingia mikataba na skimu za bima ya afya, ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora, zenye ubora na endelevu kwa wananchi wote.
Serikali imeendelea kusisitiza kuwa Bima ya Afya kwa Wote ni nguzo muhimu katika kufikia lengo la huduma za afya zilizo nafuu, sawa na zenye ubora kwa Watanzania wote, huku ikiwasihi wananchi kushiriki kikamilifu katika mpango huo kwa mustakabali bora wa afya ya jamii.

.jpeg)
0 Maoni