F CRDB foundation yazindua mpango wa mikopo isiyo na riba kwa wanawake na vijana Babati. | Muungwana BLOG

CRDB foundation yazindua mpango wa mikopo isiyo na riba kwa wanawake na vijana Babati.




Na John Walter-Babati

Benki ya CRDB kupitia CRDB Foundation imezindua rasmi mpango wa kutoa mikopo isiyo na riba kwa ajili ya uwezeshaji wa wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum, uzinduzi uliofanyika leo katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara.

Mpango huo unalenga kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia utoaji wa mitaji sambamba na mafunzo ya elimu ya fedha, ikiwa ni pamoja na namna ya kutunza fedha, kuweka kumbukumbu za biashara, kuandaa bajeti na uelewa mpana wa masuala ya fedha ili kuhakikisha mikopo hiyo inaleta tija kwa walengwa.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Meneja wa CRDB Kanda ya Kaskazini, Cosmas Saadat, amesema mafunzo ya elimu ya fedha yatakuwa endelevu kwa wanufaika ili kuwajengea uwezo wa kuendesha na kukuza biashara zao kwa ufanisi.

Amesisitiza kuwa kuchukua mkopo ni hatua ya kwanza, lakini uaminifu katika urejeshaji ni jambo la msingi ili mpango huo uendelee kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Kupitia mpango huo wa IMBEJU, CRDB Foundation imeshawezesha jumla ya vikundi 154 vya wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum, kwa kutoa mitaji yenye thamani ya shilingi milioni 456.

Kati ya hivyo, leo vikundi 12 vilivyosajiliwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati vimepatiwa mikopo isiyo na riba yenye jumla ya shilingi milioni 321 baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, amesema elimu ya fedha ni nyenzo muhimu kwa wananchi kufanya maamuzi sahihi ya kiuchumi.

Ameipongeza CRDB kwa kutoa mikopo isiyo na riba sambamba na elimu, akisisitiza kuwa mikopo hiyo irejeshwe kwa wakati ili wananchi wengine nao wanufaike.

Mheshimiwa Sillo amesema utoaji wa mikopo kwa wananchi ni moja ya ahadi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kampeni za mwaka 2025, na amewataka wajasiriamali kutokata tamaa bali kuendelea kusonga mbele kwa kuomba ushauri, kuweka kumbukumbu sahihi za biashara na kuandaa bajeti.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Kaganda, amesema wanawake ni nguzo muhimu katika utunzaji wa familia na maendeleo ya jamii, na ameikaribisha CRDB kuendelea kushirikiana na wilaya hiyo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Anna Mbogo, amesema matarajio ya halmashauri ni kuona mabadiliko chanya kwa vikundi vilivyonufaika na mikopo hiyo.

Ameeleza kuwa vikundi 12 vilivyokidhi vigezo vitaanza kupokea mikopo hiyo mara moja, huku akisisitiza uaminifu na urejeshaji wa mikopo bila “ujanja ujanja”.

Wananchi na wajasiriamali wanaonufaika na mpango huo wameishukuru serikali pamoja na Benki ya CRDB kwa hatua hiyo ya kuwapatia mikopo isiyo na riba, wakieleza kuwa itawasaidia kujikwamua kiuchumi na kuinua maisha yao.

 

Chapisha Maoni

0 Maoni