Mahakama ya Wilaya ya Kilindi imewahukumu Abdallah Ally Lusewa (31), Salehe Mohamed Lusewa (23) na Salehe Shaban Mngoya (43), wakazi wa Kijiji cha Songe Wilaya ya Kilindi, kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.
Tukio hilo lilitokea mnamo tarehe 18 Juni, 2025 majira ya saa 22:47 usiku katika Kijiji cha Songe, ambapo mfanyabiashara Faraji Hamza Dole alivamiwa dukani kwake na kuibiwa mali mbalimbali zenye thamani ya shilingi 9,490,000/=.
Baada ya tukio kuripotiwa Polisi Songe – Kilindi, upelelezi ulianza mara moja na mnamo tarehe 17 Julai, 2025 mtuhumiwa Abdallah Ally Lusewa alikamatwa na kuwatia mbaroni wenzake. Katika upekuzi uliofanywa nyumbani kwa Salehe Shaban Mngoya, zilipatikana televisheni mbili zilizoibiwa.
Baada ya upelelezi kukamilika, watuhumiwa walifikishwa Mahakama ya Wilaya ya Kilindi chini ya kesi namba CC No. 19503/2025, na leo tarehe 06 Februari, 2026, Mahakama hiyo mbele ya Hakimu Bw. Toto Casmir iliwakuta na hatia na kuwahukumu kifungo cha miaka 30 jela.

0 Maoni