Na John walter-Babati
Baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Babati
limepitisha mapendekezo ya bajeti ya shilingi bilioni 71 kwa kipindi cha mwaka
wa fedha 2026 hadi 2030, ikiwa ni sehemu ya mipango ya kuimarisha utoaji wa
huduma na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, John Noya, amesema bajeti
hiyo inahitaji usimamizi madhubuti na utekelezaji mzuri wa ukusanyaji wa mapato
ili iweze kuleta matokeo yaliyokusudiwa.
“Tusiposimamia vyema mapato yetu, bajeti haitafanya kazi
kama ilivyopangwa lakini tukisimamia kwa umakini, itawezesha utekelezaji wa
miradi ya maendeleo kwa ufanisi,” amesema Noya.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Anna Mbogo amesema kuwa
baada ya bajeti hiyo kupitishwa na Bunge, baraza la madiwani kwa kushirikiana
na wataalamu wa halmashauri litatoa ushirikiano mkubwa katika hatua za
utekelezaji ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela
Kaganda, amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa uwiano wa miradi ya maendeleo katika
kata zote, akibainisha kuwa wananchi wote wanastahili kunufaika kwa usawa.
Naye Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Regina
Ndege Qwaray, amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan,
tayari imeanza utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka
2025–2030, hivyo amezitaka halmashauri kuhakikisha mipango yao inaendana na
Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025–2050.
Amesisitiza kuwa upangaji na utekelezaji wa bajeti za
halmashauri unapaswa kulenga maendeleo endelevu yatakayoboresha maisha ya
wananchi kwa muda mrefu.
0 Maoni