F Kijiji cha Magugu Kupandisha Bei ya Vibanda vya Serikali, Mapato Yatarajiwa Kufikia Milioni 51 Kwa Mwaka. | Muungwana BLOG

Kijiji cha Magugu Kupandisha Bei ya Vibanda vya Serikali, Mapato Yatarajiwa Kufikia Milioni 51 Kwa Mwaka.


Na John Walter-Babati

Halmashauri ya Kijiji cha Magugu imependekeza kupandisha bei ya vibanda 83 vya serikali kutoka shilingi 5,000 hadi shilingi 30,000, sawa na ongezeko la asilimia 500.

Mpango huu unatarajiwa kuongeza mapato ya kijiji hadi shilingi milioni 51 kwa mwaka.

Mwenyekiti wa Kijiji, Loya Amos, amesema ongezeko la bei limechukuliwa kutokana na kuongezeka kwa gharama za maisha, hivyo ni vyema kuhakikisha vibanda vinapandishwa bei ili kijiji kiendelee kutoa huduma na kusimamia miradi ya maendeleo.

Diwani wa Kata ya Magugu, Stanley Charles, amewashauri uongozi wa kijiji kuhakikisha wananchi wanashirikishwa kwa usahihi kuhusu mapato na matumizi ya vibanda hivyo.

Amesema endapo mapato yatadhibitiwa vizuri, maendeleo ya kijiji yataimarika, michango ya wananchi itapungua, na malalamiko yatapunguzwa.

Diwani Stanley ameongeza kuwa ongezeko hili halihusishi vibanda vya wajasiriamali wa sokoni, bali ni kwa vibanda vya serikali vinavyosimamiwa na kijiji.

Uamuzi huu unalenga kuboresha usimamizi wa mapato na kuhakikisha maendeleo ya kijiji yanaendelea kwa uwazi na uwajibikaji.

 

Chapisha Maoni

0 Maoni