F Kiwanda cha Manyara Sugar chajinunulia Gari la Kisasa la Kuzima Moto. | Muungwana BLOG

Kiwanda cha Manyara Sugar chajinunulia Gari la Kisasa la Kuzima Moto.


Na John Walter-Babati

Kiwanda cha sukari cha Manyara Sugar, kilichopo kijiji cha Matufa, kata ya Magugu, wilaya ya Babati mkoani Manyara, kimenunua gari lenye mtambo wa kisasa wa kuzima moto lenye thamani ya shilingi milioni 65.1, ikiwa ni hatua ya kuimarisha usalama wa kiwanda, wafanyakazi na jamii inayokizunguka.

Akisoma taarifa ya ununuzi wa gari hilo, Afisa Uhusiano wa Kiwanda cha Manyara Sugar, John Jeu, amesema kuwa uongozi wa kiwanda umeamua kununua gari hilo kwa fedha zake kama sehemu ya uwajibikaji wa kijamii na kulinda mali pamoja na maisha dhidi ya majanga ya moto.

Ameongeza kuwa mafunzo ya matumizi ya mtambo huo yametolewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Manyara ili kuhakikisha ufanisi katika uokoaji.

Diwani wa Kata ya Magugu, Stanley Charles, amesema kiwanda cha Manyara Sugar kina mchango mkubwa kwa taifa kwa kutoa ajira nyingi za muda mfupi na mrefu, hali inayosaidia kuinua uchumi wa wananchi na maendeleo ya kata hiyo.

Kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha tani 70 hadi 80 za sukari kwa siku.

Akizindua rasmi gari hilo, Naibu Spika wa Bunge la Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Mheshimiwa Daniel Sillo, amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameifungua nchi kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, jambo linalowezesha viwanda kuwekeza zaidi katika usalama na maendeleo ya jamii.

Mheshimiwa Sillo amekipongeza kiwanda hicho kwa kuunga mkono jitihada za serikali kwa kutumia na kuzalisha nishati mbadala, pamoja na kuwasisitiza wananchi wa kata ya Magugu na maeneo ya jirani kuwekeza katika uzalishaji wa miwa kwa kuwa ni malighafi muhimu kwa uzalishaji wa sukari.

Ameongeza kuwa kiwanda cha Manyara Sugar kina manufaa makubwa kwa taifa kwa kulipa kodi, kuchangia uchumi wa nchi, na kuwezesha familia nyingi kuishi kwa furaha kupitia ajira.

Aidha, amekipongeza kiwanda kwa kununua gari hilo ambalo, licha ya kutumika ndani ya kiwanda, litawahudumia pia wananchi wa tarafa ya Mbugwe pindi yanapotokea majanga ya moto.

Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Manyara, Kamishna Gilbert Mvungi, amesema jeshi hilo limewapatia mafunzo na baadhi ya vifaa wafanyakazi wa kiwanda, akibainisha kuwa ni fahari kuona wadau kama Manyara Sugar wakishirikiana na serikali kupambana na majanga ya moto na kupanua wigo wa huduma kwa wananchi.

Hizi hapa ni picha mbalimbali wakati wa uzinduzi wa gari hilo la mtambo wa kuzima moto.






























































Chapisha Maoni

0 Maoni